Loading...

Orodha ya wakongwe 10 wanaotikisa Ligi Kuu Bara

Athuman Idd ‘Chuji’
Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikiingia katika mzunguko wa 10, wapo wachezaji 10 waliodumu na klabu zao muda mrefu na bado wanaendelea kufanya vyema katika mashindano hayo.

Uzoefu wao katika soka, umezisaidia timu zao kutoa ushindani katika Ligi Kuu na baadhi yao wanaendelea kuitumikia timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’. 

Ni wachezaji wachache wenye uwezo wa kujitunza na kucheza soka muda mrefu kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Madaraka Selemani.

Madaraka aliyecheza kwa mafanikio katika kikosi cha Simba na Taifa Stars, alistaafu soka akiwa na miaka 42 na ameingia kwenye orodha ya wachezaji waliocheza muda mrefu nchini.

Ingawa Ligi Kuu inashirikisha timu 20 za Tanzania Bara, wachezaji hao 10 wameonyesha bado tegemeo katika vikosi vyao kutokana na mchango mkubwa wanaotoa.

Rekodi za baadhi ya wachezaji hao zinaonyesha walianza kucheza Ligi Kuu zaidi ya miaka 15 wakitamba katika klabu tofauti na wengine wakihama na kurejea katika timu zao za zamani.

Wachezaji hao hawana tofauti na baadhi ya nyota wanaotamba Ulaya akiwemo kiungo wa Getafe, Sergio Sanchez mwenye miaka 39 aliyeanza kucheza soka mwaka 1999 timu ya Rayo Vallecano.

Pia yumo mshambuliaji wa Athletic Bilbao, Artz Aduriz (37) alianza kucheza Ligi Kuu Hispania mwaka 2000, amefunga zaidi ya mabao 206 katika mechi 510.

Kipa wa zamani wa Manchester United, Ben Foster (35) anacheza Watford, amecheza zaidi ya mechi 400.

Mshambuliaji nguli wa England, Jermain Defoe (36) anaitumikia AFC Bournemouth.

Kipa wa Arsenal, Petr Cech (36) na bado chaguo la kwanza licha ya kuanza kucheza soka mwaka 1999.

1. Shabani Nditi-Mtibwa Sugar

Nditi ni mmoja wa wachezaji waliodumu katika soka la ushindani tangu alipoibuliwa na Mtibwa Sugar mwaka 2002, amekuwa kwenye kiwango bora kwa takribani misimu yote.

Kiungo huyo ambaye ndiye nahodha wa Mtibwa Sugar ametimiza miaka 16 katika Ligi Kuu na bado amekuwa tegemeo katika kikosi hicho. Nditi aliwahi kucheza Simba kabla ya kurejea katika klabu hiyo.

“Mpira una mambo mengi kwa sababu unaweza ukafanya mazoezi sana na bado usipate nafasi ya kucheza, unaweza ukapata majeraha na ukaona ndio mwisho. Hiyo ipo kwa wachezaji wengi, binafsi sikukata tamaa ndio siri yangu kubwa ya kucheza muda mrefu,” alisema Nditi.

2. Juma Kaseja- KMC
Ndiye kipa aliyecheza muda mrefu zaidi miongoni mwa makipa waliopo katika vikosi mbalimbali vya timu za Ligi Kuu.

Kaseja alianza kucheza mashindano hayo mwaka 2000, alipojiunga na Moro United akitokea Makongo Sekondari kabla ya kuhamia Simba alikodumu kwa zaidi ya miaka kumi.

"Kikubwa ni kuzingatia vitu ambavyo havitakiwi katika maisha ya mpira na hapo ndio utadumu muda mrefu, kuzingatia miiko kuachana na makundi mabaya ya watu wenye mtazamo hasi juu ya maisha,”alisema Kaseja alipozungumza na gazeti hili.

Licha ya kucheza kwa miaka 20 kwenye ligi hiyo, Kaseja amekuwa katika kiwango katika timu zote alizocheza kuanzia Moro United, Simba, Yanga, Mbeya City na Kagera Sugar.

3. George Kavila-Kagera Sugar

Kiungo George Kavila anaweza kuwa ndiye mchezaji aliyecheza muda mrefu zaidi katika mashindano hayo.

Kavila alianza kucheza Ligi Kuu mwaka 1998 katika kikosi cha Coastal Union ya Tanga na amewahi kucheza katika klabu tofauti kabla ya kutua Kagera Sugar ambako ndiye nahodha.

4. Henry Joseph-Mtibwa Sugar 

Henry aliwahi kuwa nahodha wa Taifa Stars akipokea kijiti kutoka kwa Mecky Mexime. Kiungo huyo alianza kucheza ligi mwaka 2002 akiwa Mtibwa Sugar kabla ya kujiunga na Simba. Pia aliwahi kucheza soka ya kulipwa Norway.

"Wachezaji hasa chipukizi wanatakiwa kuacha makundi yasiyofaa, wanatakiwa wajielewe kwa sababu mpira ni kazi ambayo unatakiwa kuiheshimu na kujitunza,"alisema Henry.

5. Athuman Idd ‘Chuji’- Coastal Union

Kocha wa zamani wa Taifa Stars Mbrazil Marcio Maximo, aliwahi kutamka hakuwahi kumshuhudia kiungo mwenye uwezo mkubwa nchini kama Chuji.

Baada ya kutamba Makongo Sekondari na Serengeti Boys, Chuji alitua Polisi Dodoma iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu mwaka 2003. Alicheza muda mfupi kabla ya kutua Simba na baadaye Yanga.

Chuji ameacha pengo kubwa Yanga na Taifa Stars, hadi sasa hakuna mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji kama Chuji.

6. Haruna Moshi 'Boban'-African Lyon

Moshi anayetoka katika familia ya soka, alianza kucheza Ligi Kuu mwaka 2003 akiwa Moro United kabla ya kujiunga na Simba.

Kama ilivyokuwa kwa Chuji, Maximo alimtaja Boban ni mchezaji wa aina yake nchini na alikuwa na sifa zote za kucheza Ulaya kutokana na kipaji chake.

7. Salum Kanoni-Mtibwa Sugar

Beki Salum Kanoni yumo katika orodha ya wachezaji waliokula chumvi nyingi katika Ligi Kuu. Kanoni alianza kucheza soka ya ushindani mwanzoni mwa mwaka 2000. Kanoni amewahi kucheza Simba na Kagera Sugar kabla ya kujiunga na Mtibwa Sugar.

8. Jacob Masawe-Stand United

Bila shaka uongozi wa Stand United haikufanya kosa kumpa kitambaa cha unahodha Masawe, kutokana na uzoefu wake kwenye Ligi Kuu alipoanza kucheza tangu mwaka 2004 akitumika katika klabu tofauti.

9. Erasto Nyoni-Azam

Huu ni mwake wake wa 13 dimbani tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu mwaka 2005 katika kikosi cha AFC Arusha. Nyoni aliwahi kucheza soka ya kulipwa Vital O ya Burundi kabla ya kutua Azam.

Kwa sasa ni mchezaji wa Simba na Taifa Stars, akiwa ndiye mchezaji mkongwe zaidi, lakini ubora wake umempa nafasi ya kuwemo katika kikosi cha kwanza.

10. Aggrey Morris-Azam

Beki na nahodha wa Azam Aggrey Morris ni mmoja wa mabeki tegemo kwa timu yake na Taifa Stars, Aggrey alianza kucheza Ligi Kuu Zanzibar mwaka 2004 akitamba na kikosi cha Mafunzo kabla kusajiliwa na Azam mwaka 2009 alikodumu hadi sasa.
Orodha ya wakongwe 10 wanaotikisa Ligi Kuu Bara Orodha ya wakongwe 10 wanaotikisa Ligi Kuu Bara Reviewed by Zero Degree on 10/26/2018 12:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.