Loading...

Wanafunzi zaidi ya 60 wanusurika kutumbukia chooni


Zaidi ya Wanafunzi 65 wa Shule ya msingi ya Seliani jijini Arusha wamenusurika kifo baada ya choo cha shule hiyo kutitia na kuibua taharuki kwa wazazi, ambapo mtoto mmoja ameripotiwa kupata majeraha na anaendelea na matibabu katika hospitali ya Seliani.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru iliyopo mkoani humo, Jerry Murro amesema kuwa tukio hilo limetokea asubuhi majira ya saa 4, ambapo mwanafunzi mmoja amejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya wilaya.

Muro amewataka wananchi kuwa watulivu wakati wa zoezi la ufukuaji wa vifusi vilivyoporomoka katika choo hicho ili waweze kuona kama kuna wanafunzi wengine wamefukiwa ingawa inasemekana walikuwa zaidi ya mmoja ndani ya choo hicho.

"Tayari kikosi cha uokoaji kinaendelea na kazi ya kutoa vifusi ili kuangalia kama kuna wanafunzi wengine waliofukiwa, na baadaye tutaunda tume ya uchunguzi wa tukio hili ili kufahamu chanzo", amesema Muro.

Kutokana na shule hiyo kuwa na choo kimoja chenye matundu ishirini ambacho ndicho kilikuwa pekee kwa shule hiyo, imemlazimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuchukua hatua za kuzungumza na uongozi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Seliani na kuomba shule kutumia vyoo vya Kanisani hilo, ombi ambalo lilikubaliwa na Mkuu wa jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Philemon Joseph Mollel ambae aliungana na Mkuu wa Wilaya katika zoezi la uokoaji na hivyo kuondoa mashaka ya kufungwa kwa shule hiyo.
Wanafunzi zaidi ya 60 wanusurika kutumbukia chooni Wanafunzi zaidi ya 60 wanusurika kutumbukia chooni Reviewed by Zero Degree on 10/26/2018 06:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.