Loading...

Watu 20 wamepoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba mto Ruvuma


WAKAZI wapatao 20 wa kijiji cha Chapingo, Kata ya Chikolopola wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu kutokana na kushambuliwa na mamba kwenye mto Ruvuma.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na wakazi wakiongozwa na mwenyekiti wa kijiji hicho baada ya Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa kutembelea kijijini hapo.

Katika ziara hiyo ya waziri iliyolenga kukagua na kujionea maendeleo ya mradi wa maji unaotekelezwa kijiji hapo, mwenyekiti wa kijiji, Chiwonda Ally alisema vifo hivyo vimechangiwa na ukosefu wa huduma ya majisafi na salama kijijini hapo.

“Yaani kipindi hiki cha miaka mitatu wamekufa wengine wamekuwa walemavu kwa hiyo ni mwaka hadi mwaka, hivyo serikali ituangalie na kutusaidia kukabiliana na suala hili la maji maana watu tunapoteza maisha kwa sababu ya tatizo la maji na huduma ya maji kipindi chote hiki tunategemea mto Ruvuma,” alisema.

Mkazi wa kijiji cha Chapingo, Fatuma Hakika ambaye mumewe alifariki kwa kushambuliwa na mamba aliomba serikali iwasaidie kumaliza tatizo la maji. “Mume wangu alifariki kwa kushambuliwa na mamba yaani ni shida tupu watoto na wajukuu zetu, ” alisema.

Mmoja wa watu waliowahi kujeruhiwa na mamba, Mussa Bakari alisema alijeruhiwa kwenye mkono wakati akichota maji mtoni.

Bakari alisema, “Nashukuru Mungu kwa hatua hii maana wenzetu wamepoteza maisha kabisa kwa kushambuliwa na mamba kwa hiyo tunaishukuru serikali baada ya kuona tatizo hili jitihada tunaziona imetuletea maji ila sema tu mkandarasi anachelewesha kumaliza mradi.”

Waziri Mbarawa amesema Serikali haitaki kuona wananchi wakiendelea kupata shida ya maji safi na salama.

“Serikali hatuwezi kukubali wananchi wanakufa na mamba kwa ajili ya tatizo hili,” alisema.

Mradi wa maji katika kijiji cha Chapingo unaogharimu Sh bilioni tatu, ulianza mwaka 2014 na umekamilika kwa asilimia 78 huku ukitarajiwa kukabidhiwa Desemba 15 mwaka huu.

Waziri Mbarawa anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Mtwara na ameshatembelea miradi kwenye wilaya za Mtwara, Tandahimba, Newala.
Watu 20 wamepoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba mto Ruvuma Watu 20 wamepoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba mto Ruvuma Reviewed by Zero Degree on 10/22/2018 12:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.