Loading...

Bunge lajivua lawama juu ya kanuni mpya ya pensheni


BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limejivua lawama juu ya kanuni mpya ya pensheni ambayo imetangazwa hivi karibuni ya mstaafu kulipwa asilimia 50 ya mafao yake baada ya ukomo wa ajira.

Kanuni hiyo iliyotangazwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) pia inabainisha kuwa katika kiasi cha fedha kinachobaki, mstaafu huyo atalipwa kama mshahara kwa miaka 12 .

Kutokana na suala hilo ambalo limeibua mjadala mzito kila kona huku wananchi na baadhi ya wanasiasa wakipinga, Spika wa Bunge, Job Ndugai, jana aliibuka na kuweka bayana ukweli huku akisema Bunge halihusiki katika suala hilo.

Sambamba na kuweka wazi suala hilo, Ndugai pia alisema bunge linaweza kuingingilia na kuagiza kanuni hiyo ifanyiwe mabadiliko kama inaonekana ni kandamizi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Nipashe, Ndugai alisema kanuni hiyo ambayo inalalamikiwa haijatokana na chombo hicho cha kutunga sheria kwa kuwa kazi ya kutunga kanuni ni ya serikali kupitia wizara husika na sheria iliyopitishwa.

“Hii si sheria bali ni kanuni na kwa kawaida bunge lilishatunga sheria, hatua inayofuata ni kupelekwa kwa Rais kwa ajili ya kutiwa saini. Lakini kabla ya kuanza kutumika, wizara yenye dhamana na sekta husika inatunga kanuni na kuzitangaza katika Gazeti la Serikali,” alisema.

“Sasa kwa jambo hilo ambalo limeibua mjadala mzito, bunge limetwishwa mzigo mzito lisioustahili na hata watu wamefikia hatua ya kunishambulia mimi binafsi. Ukweli ni kwamba katika hili, Wizara yenye dhamana na sekta ya hifadhi ya jamii (Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ndiyo iliyotunga kanuni hiyo,” aliongeza.

Ndugai pia alimsifu Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, ambaye pia ni Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), aliyeibua suala hilo juu ya pensheni hiyo.

Alhamisi wiki hii, Bulaya aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kikokotoo hicho kipya kilichotungwa na serikali ni kitanzi kwa wastaafu kwa kuwa hawatanufaika na fedha zao ambazo wamezitolea jasho kwa miaka mingi.

“Kwa kweli alichokisema Mheshimiwa Bulaya ni kweli na ameweka wazi kwamba imetokana na serikali na bunge halihusiki,” alisema.

Katika taarifa yake kwa wanahabari, Bulaya alikaririwa akisema: “Wabunge tulitaka kikokotoo kiwepo kwenye sheria, lakini kwa masikitiko makubwa bungeni tuliambiwa kuwa ni kanuni ambayo inampa waziri ambaye yuko kwa maslahi ya serikali.”

Bulaya aliongeza kuwa, hata wadau waliwataka wabunge wakijue kikokotoo hicho na waliomba kisiwe 1/580 bali kiwe 1/540 au pungufu, lakini kilifichwa na hakikujulikana kwa watunga sheria hao.

Pamoja na bunge kutowekwa wazi, kwa mujibu wa Bulaya, SSRA hivi karibuni iliweka bayana suala hilo na hatimaye kuibua mjadala mzito kila kona huku baadhi ya wananchi wakisema ni ukandamizaji dhidi ya wastaafu.
Bunge lajivua lawama juu ya kanuni mpya ya pensheni Bunge lajivua lawama juu ya kanuni mpya ya pensheni Reviewed by Zero Degree on 11/25/2018 03:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.