Tarehe ya Uchaguzi Yanga yatajwa
Kumekuwa na mvutano tangu klabu hiyo kutakiwa kuitisha uchaguzi wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi, huku baadhi ya wanachama wakitaka aliyekuwa Mwenyekiti wao Yusuf Manji arejee lakini hakuonyesha ushirikiano.
Hivi karibuni viongozi wa Yanga walikutana na Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe kujadili suala la uchaguzi na baadae Baraza la Michezo la Taifa, lilikuja na uamuzi wa kuitaka TFF isimamie klabu hiyo ifanye uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela, alisema Yanga watafanya uchaguzi wa kujaza nafasi zilizoachwa ikiwamo ya mwenyekiti , makamu mwenyekiti na wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji.
Mchungahela alisema mchakato wa uchaguzi huo tayari umeanza na utasimamiwa na kamati hiyo, pamoja na kamati ya uchaguzi ya Yanga.
Alitaja utaratibu wa mchakato huo kuwa Novemba 5-7, mwaka huu, kutangaza mchakato wa uchaguzi, Novemba 8-13 wagombea wataanza kuchukua fomu, Novemba 14-17 ni kikao cha mchujo wa awali.
Tarehe 18-20 ya mwezi huo, kuchapisha na kubandika orodha ya awali ya wagombea katika ubao wa matangazo, Novemba 21-24, kipindi cha kupokea na kuweka mapingamizi.
Alieleza kuwa Novemba 24-27 kupitia pingamizi zote na kufanya usaili wa wagombea, tarehe 28-30 kutangaza na kubandika matokeo ya awali ya usaili.
“Tarehe 1-4 Desemba sekretarieti ya TFF, kuwasilisha masuala ya maadili katika kamati ya maadili ya TFF, Desemba 5-10 kipindi cha kupokea na kutolea maamuzi ya kamati ya maadili, ” alisema.
Alifafanua kuwa mchakato huo utaendelea kwa kufuata hatua kwa hatua hadi Januari 6, mwakani kampeni zitakapoanza mpaka tarehe 13 ya uchaguzi.
“Mambo yote hayo yatasimamiwa na kamati ya uchaguzi ya TFF kwa kufuata Katiba kwa kuwa Yanga ni mwanachama wa TFF,” alisema Mchungahela.
Tarehe ya Uchaguzi Yanga yatajwa
Reviewed by Zero Degree
on
11/06/2018 07:50:00 AM
Rating: