Loading...

Modric akomesha utawala wa Messi na Ronaldo tuzo ya Ballon d'Or


Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa la Croatia Luka Modric ameshinda tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka 2018, na kuwa mchezaji wa kwanza tofauti na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kushinda tuzo hiyo baada ya miaka 10.

Ronaldo & Messi walitawala kuanzia 2008

Modric, 33, ameshinda kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei kwa mara ya tatu mfululizo na kulisaidia taifa lake kufika hatua ya fainali katika michuano ya Kombe la Dunia.

Mchezaji wa zamani wa Brazil na AC Milan Kaka, alishinda tuzo hiyo mwaka 2007, na baada ya hapo Messi na Ronaldo wameshinda mara tano kila mmoja tuzo hiyo ya thamani kabisa kwa wachezaji wa kandanda duniani.

Ronaldo, ambaye amehamia Juventus msimu huu amemaliza katika nafasi ya pili mwaka huu, huku Messi akishika nafasi ya tano. Nafasi ya tatu ameshika mshambuliaji wa Atletico Madrid Antoine Griezmann huku mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe akishika nafasi ya nne - wawili hao walikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichoshinda Kombe la Dunia mwaka huu.

Huu umekuwa mwaka wa kutuzwa kwa Modric ambaye awali alishinda tuzo ya FIFA ya mchezaji bora wa kiume na pia alishinda tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa taarifa ya BBC, Modric amesema tuzo yake ni zawadi kwa wachezaji wote ambao waliikosa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

"Labda huko nyuma kuna wachezaji ambao walistahili kushinda Ballon d'Or kama Xavi, Andres Iniesta au [Wesley] Sneijder lakini sasa watu wameamka a wanaanza kuangalia wachezaji wengine," amesema.

"Huu umekuwa mwaka wa kipekee sana kwangu. Ni vigumu kuzielezea hisia zangu kwa maneno. Ni kitu cha pekee sana kwangu."

Modric amewasifia Ronaldo na Messi kama "wachezaji bora kabisa", na kuongeza "hivyo ushindi wangu huu unamaanisha kuwa nimefanya vitu vikubwa sana uwanjani mwaka huu, na ndio maana 2017-18 umekuwa ni mwaka wangu."

Mohammed Salah ndiyo mchezaji pekee kutoka Afrika aliyeingia katika 10 bora kwa kushika nafasi ya sita, na ndiyo mchezaji kinara kutoka ligi ya premia ya England.

Modric alikuwa ni miongoni mwa wachezaji nane wa Real Madrid kati ya wachezaji 30 waliokuwa wakiwania tuzo hiyo, akiwemo Gareth Bale aliyemaliza katika nafasi ya 17.

Mshambuliaji wa Lyon na Norway Ada Hegerberg, 23, ameshinda tuzo ya kwanza ya Ballon d'Or kwa wachezaji wa kike huku Mbappe,19, akishinda tuzo ya Kopa inayotolewa kwa mchezaji bora chini ya miaka 21 kwa kupigiwa kura na washindi wa zamani wa Ballon d'Or.



10 Bora ya Ballon d'Or


1. Luka Modric (Real Madrid na Croatia)

2. Cristiano Ronaldo (Juventus 
na Ureno)

3. Antoine Griezmann (Atletico Madrid 
na Ufaransa)

4. Kylian Mbappe (Paris St-Germain 
na Ufaransa)

5. Lionel Messi (Barcelona 
na Argentina)

6. Mohamed Salah (Liverpool 
na Misri)

7. Raphael Varane (Real Madrid 
na Ufaransa)

8. Eden Hazard (Chelsea 
na Ubelgiji)

9. Kevin de Bruyne (Manchester City 
na Ubelgiji)

10. Harry Kane (Tottenham 
na Uingereza)
Modric akomesha utawala wa Messi na Ronaldo tuzo ya Ballon d'Or Modric akomesha utawala wa Messi na Ronaldo tuzo ya Ballon d'Or Reviewed by Zero Degree on 12/04/2018 07:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.