Loading...

Ajali 9 kubwa za ndege zilizotikisa dunia


Usafiri wa ndege unatajwa kuwa ndiyo salama kuliko usafiri wa aina nyingine duniani ikiwamo wa majini na barabara.

Hata hivyo, matukio tisa ya ajali kubwa za ndege zilizo tokea ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita yameleta mshtuko mkubwa na maswali mengi. 

Uchambuzi wa matukio nane uliofanywa na gazeti hili kwa msaada wa taarifa ya Machi 11 mwaka huu katika tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), unabainisha ajali hizo zilizotokea kati ya mwaka 1999 hadi 2019 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100 katika kila ndege.

Uchambuzi huo umefanyika siku tatu zikiwa zimepita tangu kutokea kwa ajali ya ndege aina ya Boeing 737 Max 8 ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kusababisha vifo vya watu 157 wakiwamo wafanyakazi wa ndege hiyo.

Ajali hiyo imezusha hofu juu ya usalama wa ndege aina ya Boeing 737 MAX 8 na kupelekea mashirika mengi kufuta safari za ndege hizo.

Itakumbukwa kuwa Oktoba 29 mwaka jana ndege aina ya Boeing 737 Max ilipata ajali katika Bahari ya Java dakika chache baada ya kuruka kutoka jiji la Jakarta, Indonesia na abiria wote 189 na wafanyakazi walifariki dunia sababu za kiufundi zikitajwa kuwa chanzo cha ajali hiyo.

Aprili 11 mwaka huo, ndege ya kivita ya Algeria ilipata ajali karibu na makao makuu ya nchi hiyo Algiers. Baadhi ya mashuhuda walisema waliona bawa likiwaka moto dakika chache baada ya kuruka. Abiria wote 257 ambao ni wanajeshi na familia zao walifariki dunia.

Oktoba 31 2015, ndege aina ya Airbus A321 ya Shirika la Ndege la Kogalymavia la Urusi ilipata ajali eneo la Penisula ya Sinai dakika 22 baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Sharm el-Sheikh, Misri na kuua abiria wote 224. Baadaye kundi la waasi la Islamic State la Syria lilitangaza kuhusika.

Julai 24, 2014 ndege aina ya Air Algérie Flight 5017 ikitokea Ouagadougou, Burkina Faso kuelekea Algiers, Algeria ilipotea eneo la mpakani mwa Burkina Faso na Mali kutokana hali mbaya ya hewa na baadaye ilipatikana imeanguka na kuua abiria wote 116, kati yao Wafaransa wakiwa 51.

Julai 17, 2014 ndege aina ya MH17 ya Shirika la Ndege la Malaysia ilipata ajali Mashariki mwa Ukraine na kuua abiria wote 298. Kundi la wapiganaji waliokuwa wakiipinga Serikali ya Urusi lilituhumiwa kuhusika.

Desemba 28, 2014 ndege aina ya AirAsia QZ8501 iliyokuwa ikitokea Surabaya, Indonesia kwenda Singapore ilipotea eneo la Bahari ya Java baada ya rubani kujaribu kukwepa hali mbaya ya hewa lakini akashindwa. Abiria 162 walifariki dunia.

Aprili 20, 2012 ndege aina ya Boeing 737 ya Shirika la Ndege la Bhoja, Pakistani ilipata ajali wakati ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Islamabad kwa sababu ambazo hazikufahamika na abiria wote 121 walifariki.

Juni 30, 2009, ndege aina ya Airbus 310 ikiwa na abiria wa Yemeni ilipata ajali katika ukanda wa Bahari ya Hindi karibu na visiwa vya Comoro. Abiria mmoja kati ya 153 alinusurika kufa.

Dosari za kiufundi pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa yalibainika kuwa chanzo kikubwa cha ajali nyingi za ndege zilizotokea katika kipindi hicho cha miaka 10 iliyopita.




Chanzo: Mwananchi
Ajali 9 kubwa za ndege zilizotikisa dunia Ajali 9 kubwa za ndege zilizotikisa dunia Reviewed by Zero Degree on 3/13/2019 11:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.