Loading...

Mikoa inayoongoza kwa uchafuzi wa noti nchini



Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeitaja mikoa ya Kigoma na Kagera kuwa ndiyo inayoongoza kwa kuwa na noti chakavu na kuwataka wenye fedha hizo au zilizoharibika kuzibadilisha kwenye matawi ya benki za biashara.

Meneja msaidizi wa uhusiano kwa umma wa BoT, Victoria Msina alisema jana mjini Kigoma kuwa wakazi wa mikoa hiyo wanaongoza kwa uchafuzi wa noti wakifuatiwa na wa Mkoa wa Kagera.

“Utafiti tuliofanya tumebaini mikoa ya Kigoma na Kagera inaongoza kwa kuchafua noti. Fedha zinachakaa mno ukilinganisha na mikoa mingine, ndiyo maana tumeamua kutoa elimu kuanzia na mikoa hii miwili,” alisema Msina wakati wakizungumza na wananchi mjini hapa.

BoT inatoa elimu ya umuhimu wa kutunza fedha ili kuepuka uchakavu sambamba na utambuzi wa alama ili kutofautisha noti halali na bandia kwa urahisi.

Diwani wa Kigoma Mjini, Hussein Kalyango alisema noti nyingi zinazotumika mkoani humo ni vigumu kuzitumia katika mikoa mingine.

“Kuna noti tunazitumia hapa Kigoma lakini ukifika nazo Dar es Salaam utaambiwa ni mbovu na hawazipokei. Kwa hiyo ni lazima BoT mtoe elimu kwa jamii ili wajue umuhimu wa kutunza noti zisichakae mapema,” alisema Kalyango.

Meneja msaidizi wa utunzaji fedha na alama za usalama wa BoT, Abdul Dollah aliwaambia wakazi wa mji huo kuwa benki za biashara zimepewa jukumu la kubadilisha fedha chakavu.

Alisema benki hizo zimepewa jukumu la kupokea fedha chakavu kutoka kwa wananchi, kisha kuzipeleka BoT kwa ajili ya hatua ya uteketezaji.

“Benki zote sasa zinapokea fedha mbovu na chakavu na (mwananchi) utabadilishiwa kwa kupewa fedha nzima bila kukatwa, lengo ni kupunguza usumbufu unaojitokeza,” alisema Dollah.

Aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuuza noti mbovu au chakavu kwa watu wanaozinunua kwa gharama ndogo kwa kuwa hata wao huzipeleka kwenye benki za biashara kuzibadilisha kwa thamani halisi.

Mfanyabiashara wa Soko la Kigoma, Mathias John alisema mpango wa kubadilisha noti chakavu utasaidia kupunguza fedha mbovu zilizopo kwenye mzunguko.

Watumishi wa BoT wapo mkoani humo kwa ziara ya siku tano kuelimisha jamii juu ya utunzaji bora wa noti na wanatarajia kutembelea wilaya za Uvinza na Kasulu. Wananchi wa Kigoma Mjini wanaweza kubadilisha fedha chakavu katika benki za CRDB, NMB, NBC, TPB na Exim zilizopo mkoani humo.


Chanzo: Mwananchi
Mikoa inayoongoza kwa uchafuzi wa noti nchini Mikoa inayoongoza kwa uchafuzi wa noti nchini Reviewed by Zero Degree on 3/08/2019 07:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.