Loading...

Waziri: Kujiunga JKT si uhakika wa ajira


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi amelieleza Bunge kuwa programu ya mafunzo kwa vijana inayotolewa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), haiwahakikishii ajira katika taasisi hiyo bali inawaandaa kujitegemea na kujiajiri.

Waziri Mwinyi ameyabainisha hayo leo, Jumanne (Mei 28, 2019) bungeni, Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Angelina Malembeka aliyehoji uwepo wa manung’uniko ya vijana kukosa ajira hasa upande wa jinsia ya kike katika wilaya za Kaskazini ‘A’ na Kaskazini ‘B’ huko Zanzibar.

‘’Lazima vijana waelewe kuwa sio ajira, kujiunga JKT ni kwenda kujifunza mafunzo ya kijeshi pamoja na stadi za kazi….Tunachukua takribani vijana elfu 20 kwa mwaka, vyombo vya ulinzi na usalama havina uwezo wa kuchukua wote hao katika ajira,’’ alisema Dk Mwinyi.

Akifafanua zaidi, Dk Mwinyi amesema kuwa jukumu la ugawaji wa nafasi hizo za mafunzo halipo chini ya Wizara yake bali ni suala ambalo lipo chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo imekuwa ikipanga idadi ya vijana wanaotakiwa kujiunga kwa kila wilaya.

Waziri Mwinyi ameeleza uchache wa jinsia ya kike wanaojiunga na JKT unatokana na uchache wao wakati wa usaili huku baadhi wakikosa sifa zinazohitajika.

Alieleza kigezo kingine kinatokana na uwiano wa idadi wakazi wa maeneo husika kwa kuzingatia sense ya Watu na Makazi. Wakati huohuo, Waziri Mwinyi amewataka vijana wanaojiunga na JKT kuwaza zaidi kujiajiri baada ya mafunzo pamoja na kutafuta ajira katika sekta binafsi kwa kuwa “kujiunga na JKT haitoi moja kwa moja fursa ya kuajiriwa.”

Chanzo: Habari Leo
Waziri: Kujiunga JKT si uhakika wa ajira Waziri: Kujiunga JKT si uhakika wa ajira Reviewed by Zero Degree on 5/28/2019 09:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.