Loading...

Shahidi amtaja Okwi kesi ya akina Aveva


MHASIBU Mkuu wa Simba, Amos Juma, amedai fedha za kumuuza mshambuliaji wa timu hiyo, Emmanuel Okwi kwenda Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, Dola za Marekani 300,000 zilihamishiwa kwenye akaunti ya aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva, kinyume na makubaliano ya kikao cha kamati ya utendaji.

Hayo yalidaiwa jana na shahidi huyo wa sita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali wa Takukuru, Leonard Swai, shahidi huyo, alidai Machi 14, 2016 kiliitishwa kikao cha Kamati ya Utendaji cha kawaida kikiwa na ajenda 10, ikiwamo ya mauzo ya Okwi ambayo ilikuwa ya saba.

Alidai fedha za kumuuza Okwi zilikuwa ni Dola 319, 212 ambapo Aveva alizitolea taarifa katika kikao na kamati ili ijadili fedha hizo.

“Ajenda katika kikao zilikuwa tatu, ajenda ya kwanza fedha hizo zitumike katika ujenzi wa uwanja wa Klabu ya Simba uliopo Bunju, pili, Zackaria Hanspoppe alipwe deni lake Dola za Marekani 17,200 na fedha nyingine ziwekwe katika akaunti maalumu kwa ajili ya uwanja wa Bunju.

“Juni 16, 2016 nikiwa ofisini kwangu, Makamu wa Rais, Godfrey Nyange (Kaburu) alikuja kuomba nimpe kitabu cha hundi ya akaunti ambayo fedha za Okwi ziliingizwa, nilimpa lakini alipokirudisha karatasi mbili hazikuwepo.

“Alinikabidhi kipande cha karatasi kikionesha kuna Dola za Marekani 300,000 zilizohamishiwa katika akaunti ya Aveva, karatasi hiyo ilitoka Benki ya CRDB.

“Baada ya kunikabidhi niliomba maelezo kwa Nyange, alinipa maelezo nikaandaa tamko ili kuweka kumbukumbu,” alidai shahidi.

Alidai Nyange alidai fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo kwa ajili ya miradi ya Simba, zitatolewa kupitia bajeti iliyopitishwa na kamati ya utendaji na matumizi yake yatapitishwa na kamati hiyo.

“Muhtasari wa kikao cha Kamati ya Utendaji hakikuelekeza fedha hizo kuhamishiwa katika akaunti ya Aveva,” alidai.

Alidai kiuhasibu ilikuwa vigumu kushughulikia fedha zilizowekwa katika akaunti ya mtu binafsi.

Shahidi alidai baada ya fedha kuingizwa katika akaunti ya Aveva, kiasi kingine kilihamishiwa katika akaunti ya Kampuni ya Nina kwa ajili ya kuagiza nyasi, alilipwa mkandarasi wa ujenzi wa uwanja wa Bunju, kiasi kingine kwa ajili ya kibali cha kuruhusu ujenzi na Dola za Marekani 17,000 alilipwa Hanspoppe.

Anadai hajawahi kuona nyaraka yoyote ikionyesha Aveva anaidai Klabu ya Simba na kwamba malipo kwa ajili ya kukomboa nyasi bandia bandarini yalilipwa kwa awamu mbili tofauti.

“Mara ya kwanza zililipwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania Shilingi milioni 82 na mara ya pili Shilingi milioni 85 kwa ajili ya kutoa nyasi,” alidai.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na 16, 2016 Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya ofisi.

Chanzo: Bingwa
Shahidi amtaja Okwi kesi ya akina Aveva Shahidi amtaja Okwi kesi ya akina Aveva Reviewed by Zero Degree on 6/27/2019 08:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.