Loading...

Chadema wajibu madai kuhusu uenyekiti wa Mbowe


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekiri kupokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na kusema kuwa chama hicho hakijakiuka Sheria yoyote kama ambavyo ilikuwa imenukuliwa.

Kupitia taarifa iliyotolewa jana Oktoba 3, 2019 na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya chama hicho Tumaini Makene, imesema kuwa Katiba ya chama hicho inatoa mamlaka kwa kamati, kusogeza mbele uchaguzi mkuu ndani ya chama.

"Tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa chama, inaweza kurekebishwa kwa kusogezwa mbele kwa muda usiozidi mwaka mmoja, toka mwisho wa uhalali wa uongozi uliopo, Mamlaka ya kufanya marekebisho haya yameachwa kwa Kamati Kuu" imeeleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa Kamati kuu ya chama hicho, ilikaa katika kikao chake cha tarehe 27 na 28, Julai, 2019 na kurekebisha ratiba ya uchaguzi, ambapo utakamilika mwezi Disemba kwa ngazi ya Taifa na kwamba kwa sasa kinaifanyia kazi barua hiyo ili iweze kuifikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ndani ya muda husika.

Hatua hii imekuja baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kusema kuwa uongozi wa chama hicho chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, umemaliza muda wake tangu Septemba 14, 2019 na kukitaka kuandika maelezo ya kwanini kisichukuliwe hatua baada ya kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na kuwataka wawasilishe maelezo hayo Oktoba 7, majira ya saa 9:30 jioni.
Chadema wajibu madai kuhusu uenyekiti wa Mbowe Chadema wajibu madai kuhusu uenyekiti wa Mbowe Reviewed by Zero Degree on 10/04/2019 08:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.