Loading...

Mvua zasababisha kizaazaa jijini Dar


WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam jana walijikuta katika wakati mgumu baada ya kukwama kupata usafiri, nyumba kufurika maji huku maeneo mengine yakishindwa kupitika.

Maeneo yameonyesha barabara nyingi kujaa maji ya mvua na kushindwa kupitika kirahisi.

Makutano ya barabara ya Goba na Bagamoyo, maji yalionekana kujaa hali iliyosababisha watumiaji wa barabara hiyo kushindwa kuitumia baada ya kingo za barabara hiyo kufunikwa na maji hayo.

Eneo la Jangwani, wakazi wanaozunguka Mto Msimbazi, nyumba zao zilizingirwa na maji hayo yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika jiji la Dar es Salaam.

Watu wa eneo hilo walilazimika kutembea kwa miguu kutokana na kusekana kwa usafiri kutokana na barabara inayopitia Jangwani kufunikwa na maji hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa eneo hilo, walisema miongoni mwa sababu zinazochangia mafuriko hayo ni pamoja na takataka kujaa kwenye Mto Msimbazi na kushindwa kupitisha maji kipindi cha mvua.

Jumanne Bushiri, mkazi wa eneo hilo, Kata ya Magomeni, alisema bila serikali kuchukua hatua za haraka, kuna hatari ya kutokea madhara makubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza na Nipashe, Mjumbe wa Baraza la Usuluhishi katika kata hiyo, Habiba Mondoma, alisema ni vyema mpango wa kuendeleza mto huo ukafanyika haraka ili kuokoa wananchi wake.

"Tunajua kwamba kuna mpango wa kuendeleza Bonde la Mto Msimbazi, na hii ndiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wakazi wanaouzunguka, kwa sababu nyumba nyingi zinajaa maji kutokana na kukosa pa kwenda, badala ya kwenda Msimbazi yanaingia kwenye nyumba za watu,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema wakazi kutoka kata 18 zinazouzunguka mto huo nyumba zao zimejaa maji na kulazimika kukimbia kwa muda.

"Hivi ninavyozungumza na wewe, nyumba nyingi kutoka katika kata hizi zinazozunguka Mto Msimbazi, zimejaa maji, wakazi wamelazimika kukimbia katika nyumba zao kupisha maji mpaka yatakapopungua," alisema Mondoma.

"Tunaiomba Wizara ya Fedha itoe fedha ili mradi huu wa kuboresha Mto Msimbazi uendelee, na sisi tupo tayari kulipwa fidia ili tuondoke, tunaamini pesa zipo, tunaomba watusaidie, hizi mvua ni za vuli tu, bado masika na huenda zikaleta madhara kuliko haya."

Eneo la Tandale, Mto Ng`ombe ulifurika maji na kupita juu na kuleta adha kubwa kwa wakazi wa eneo hilo pamoja na vyombo vya usafiri.

Ramadhani Majuto mkazi wa eneo hilo ni miongoni mwa wananchi waliolazimika kukaa pembeni kusubiri maji yapungue ili wavuke.
Mvua zasababisha kizaazaa jijini Dar Mvua zasababisha kizaazaa jijini Dar Reviewed by Zero Degree on 10/18/2019 08:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.