Loading...

NECTA yaeleza jinsi uvujaji wa mitihani unavyotafuna mabilioni


BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) limesema kuwa serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa kutokana na uvujaji wa mitihani.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, andiye aliyebainisha ukubwa wa gharama za kutunga mtihani mpya kwa kutolea mfano kwa shule za msingi kuwa Sh. bilioni 100 zimekuwa zikitumika kutunga na kuchapisha mtihani wa shule hizo.

Kufuata hali hiyo, amewataka walimu kuzingatia uadilifu katika usimamizi wa mitihani ili waweze kuinusuru serikali kupata hasara hiyo.

Akizungumza jana jijini hapa katika kikao cha dharura cha Baraza la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania (CWT), alisema sheria ya mtihani kuvuja ni lazima ufutwe, hivyo ili kunusuru upotevu wa fedha, na kwamba ni lazima walimu ambao ni maofisa wasimamizi wa mitihani wazingatie maadili ya kazi katika usimamizi wa mitihani.

"Walimu ni watu muhimu sana katika mitihani, hivyo mkiwa waaminifu mtafanya taifa liwe na heshima katika sekta ya elimu hususani katika mitihani inayofanyika," alisema Dk. Msonde.

Alisema lengo lao ni kuona Taifa linapata heshima ya kutuvujisha mitihani jambo ambalo linawapa heshima walimu pamoja na taifa kwa ujumla kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kinaongezeka, lakini kwa akili zao.

Akizungumzia malalamiko ya posho za walimu ambao ni maofisa wasimamizi wa mitihani, Dk. Msonde alisema utungaji wa mitihani na usimamizi hauna posho na kama ipo ni ya siri, na kuwa huwa haitangazwi wala kujulikana katika vyombo vya habari kwa sababu tukio lenyewe ni la siri.

"Mtihani ni siri hata malipo yake kama yapo ni siri na kiwango hakipaswi kujulikana kwa sababu ni tukio maalumu linapaswa kubaki siri," alisema Dk. Msonde.

Akizungumzia suala la uhakika wa vyeti vya walimu, Dk. Msonde alisema kati ya walimu 290 ambao ni wanachama wa CWT waliofanyiwa uhakiki, ni walimu 30 ndio walikutwa na vyeti feki, lakini kati ya hao walimu sita walikata rufani, ambapo mmoja kati yao ndiye alifanikiwa kurejeshwa kutokana na yalifanyika makosa.

"Kazi ya uhakiki ilikuwa ngumu sana kwa sababu wengi waliokuja kukata rufani walikuja na vyeti vingine ambavyo ni tofauti vilivyowasilishwa na waajiri wao," alisema Dk. Msonde.

Aliongeza: "Ukiacha hayo nawapongeza CWT kutokana na heshima ya maadili ya kazi wanayozidi kuionyesha na kuipa heshima sekta ya walimu. Naomba niwapongeze CWT kutokana na mnavyosimamia maadili, safari hii mitihani iko vizuri mmefanya baraza lionekane kuwa na heshima."

Kwa upande wake, Rais wa CWT, Leah Ulaya, alimshukuru Dk. Msonde kwa ufafanuzi alioutoa kuhusiana na madai ya posho za usimamizi wa mitihani na kuwataka kuwa wavumilivu kwa sababu ni siri.

Hata hivyo, CWT wameiomba serikali kusimamia suala la upandishwaji madaraja ambao inaenda sambamba na upandishwaji mishahara.

Leah alisema walimu wengi wamekuwa wakipandishwa madaraja, lakini mshahara haupandi huku mwalimu mlengwa akiendelea kutumikia nafasi hiyo kwa muda mrefu.

"Tunaomba serikali isimamie hilo, tukipandishwa daraja na mishahara upande," alisema Leah.

Chanzo: Nipashe
NECTA yaeleza jinsi uvujaji wa mitihani unavyotafuna mabilioni NECTA yaeleza jinsi uvujaji wa mitihani unavyotafuna mabilioni Reviewed by Zero Degree on 10/21/2019 07:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.