Loading...

Rugemalira, Seth wakubali yaishe

Wafanyabiashara Harbinder Sethi na James Rugemalira wakiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza, baada ya kesi inayowakabili ya uhujumu uchumi kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa mfanyabiashara, James Rugemalira ameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuomba kukiri makosa yao ya uhujumu uchumi.

Pia, mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habinder Sethi, imedaiwa aliandika barua muda mrefu tangu Rais John Magufuli alivyomuelekeza DPP kutoa msamaha kwa washtakiwa wenye mashtaka ya uhujumu uchumi ambao watakiri kosa na kurejesha hasara waliyosababisha.

Wakili wa Rugemalira, Michael Ngaro, alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kuwa mshtakiwa huyo ameandika barua ya kukiri na kwamba mpaka sasa hawajapata majibu.

Ngaro aliuomba upande wa mashtaka kufanya mchakato ili wapate majibu ya barua hiyo haraka.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simoni, alidai ni kweli wamepokea barua ya mshtakiwa wa pili (Seth) na kwamba wanaishughulikia na atapatiwa majibu.

Inadaiwa awali, Rugemalira aliandika barua ya kutaka kuonana na DPP, lakini baadaye aliamua kuandika barua ya kukiri ili kuingia kwenye makubaliano.

Hakimu Shaidi, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.Seth na Rugemalira wako gerezani kwa mwaka wa tatu, wakisubiri upelelezi wa kesi yao kukamilika.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwamo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27. Kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014, jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Pia, inadaiwa katika mashtaka ya kujipatia fedha, kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao makuu ya Benki ya Stanbic, Kinondoni na Benki ya Mkombozi, tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai washtakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309, 461,300,158.27.

Vile vile, washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara na inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati Kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti ya Dar es Salaam kwa pamoja walidaiwa kutenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni Dola za Marekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4, wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

WAACHIWA HURU


Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Rose Ngoka, jana aliwaachiwa huru washtakiwa watatu waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya utoroshaji madini ya Sh. milioni 958, baada ya kulipa faini Sh. milioni 100 na fidia Sh. milioni 10.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Ngoka alisema kulingana na makubaliano ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), mshtakiwa wa tatu, Bakari Kunga, aliyehukumiwa kulipa Sh. milioni 110 kwa awamu saba, ameshalipa awamu ya kwanza Sh. milioni 10 ya faini na fidia Sh. milioni 10 na kubakiza Sh. milioni 90, mahakama imemwachia huru.

Ngoka alisema pamoja na kumwachia huru, mshitakiwa huyo atatakiwa kulipa Sh. milioni 15 kila mwezi na kuhakikisha anamaliza kulipa fedha hizo Aprili 10, mwakani.

“Pamoja na kuachiwa huru, mahakama imeamuru hati ya nyumba yake namba 125 yenye hati namba 11394 iliyoko Kitalu E eneo la Njiro Jijini Arusha itaendelea kushikiliwa na DPP hadi atakapokamilisha kulipa fedha hizo,” alisema.

Hakimu Ngoka alisema endapo mshtakiwa huyo atashindwa kulipa fedha hizo, DPP atachukua uamuzi kwa sababu anao uwezo kisheria wa kufanya hivyo.

Kwa upande wa washtakiwa Latifa Mwarengwa na Josephat Shayo, alisema wamelipa Sh. milioni 45 kila mmoja, hivyo mahakama kuwaachia huru.

Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Mawakili wa Utetezi Anold Ojare na Said Amour, waliiambia mahakama hiyo kuwa upande wa Jamuhuri na utetezi waliushakubaliana kuwa fedha hizo zilipwe kwa awamu saba na tayari washtakiwa wameshatimiza makubaliano hayo, hivyo kuomba mahakama iwaachie huru.

Wastakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya kutorosha madini kilo 31.59 yenye thamani ya Dola za Kimarekani 416,577.58 sawa na Sh. milioni 958 Madini hayo yalikuwa aina ya tanzanite, sapphire, spinel, ruby, tourmaline, tsavorite, grossular na Aquamarine na yalikuwa yakitoroshwa kwenda nchini Kenya yakiwa kwenye gari namba T.645 DBY aina ya Suzuki Swift.

Chanzo: Nipashe
Rugemalira, Seth wakubali yaishe Rugemalira, Seth wakubali yaishe Reviewed by Zero Degree on 10/11/2019 12:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.