Loading...

Sababu ya Mdee kushindwa kuhudhuria kesi yatajwa


Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi inayomkabili baada ya gari lake kuharibika.

Hayo yameelezwa mahakamani hapo leo Jumanne Oktoba 29, 2019 na Fareson Rukomo ambaye ni mdhamini wa mbunge huyo.

Mbunge huyo anakabiliwa na kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon amedai shauri hilo lilikuja kwa ajili ya usikilizwaji, kwamba shahidi waliyekuwa wakimtegemea hajafika mahakamani sambamba na mshtakiwa.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alimtaka Rukomo kuieleza mahakama sababu za mbunge huyo kutofika mahakamani.

Mdhamini huyo alidai gari la Halima Mdee limeharibika kati ya Dodoma na Morogoro wakati akienda jijini Dar es Salaam.

"Nimepigiwa simu jana usiku wakati Mdee anakuja Dar es Salaam kwamba gari lake limeharibika kati ya Dodoma na Morogoro. Kanituma nije hapa kueleza,” amesema Rukomo.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8, 2019.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa, ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.

Chanzo: Mwananchi
Sababu ya Mdee kushindwa kuhudhuria kesi yatajwa Sababu ya Mdee kushindwa kuhudhuria kesi yatajwa Reviewed by Zero Degree on 10/29/2019 07:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.