Loading...

Serikali kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo 2030


SERIKALI inaandaa mkakati wa kitaifa wa kudhibiti kichaa cha mbwa, wenye lengo kuu la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030. Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Aliwapongeza wanaoshiriki katika kudhibiti kichaa cha mbwa nchini Alisema mkakati unaoandaliwa, unasisitiza ushirikiano wa sekta mtambuka katika kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa nchini, kama vile kuchanja mbwa na kuhakikisha chanjo ya binadamu inapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya. Pia, kutoa elimu kwa umma ya njia mahususi za kujikinga na kichaa cha mbwa.

Alisema wizara yake inaandaa mkakati huo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika Linaloshughulika na Afya ya Wanyama Duniani (OIE) na asasi zisizo za kiserikali kupitia uratibu wa Dawati la Afya Moja.

Alisema mkakati huo unaandaliwa kwa sababu ugonjwa wa kichaa cha mbwa hauna tiba. Alisema ugonjwa huo husababisha vifo na huleta athari zingine kubwa katika uchumi.

Kwamba kwa bara la Afrika, gharama ya chanjo kwa binadamu ni Sh 150,000 kwa mgonjwa, ambazo ni kiasi kikubwa. Akielezea ugonjwa huo, alisema ugonjwa wa kichaa cha mbwa uliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwaka 1932. Kwamba baada ya hapo, wagonjwa wameendelea kuripotiwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa viwango tofauti.

Ummy alisema kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, watu 16,290 wametolewa taarifa ya kuumwa na mbwa na vifo nane vimeripotiwa.

“Tatizo la kichaa cha mbwa ni kubwa zaidi, kwani takwimu hizi hazijumuishi vifo vinavyotokea nyumbani na waathirika ambao hawakufika katika vituo vya kutolea huduma za afya,” alisema.

Kwamba utafiti uliofanyika mwaka 2002 nchini Tanzania, ulibainisha kuwepo takriban vifo 1,499 kwa mwaka kutokana na ugonjwa huo. Aidha, tafiti zimeonesha waathirika wakuu wa ugonjwa huo ni watoto chini ya miaka 15, kwa sababu huwa karibu zaidi na mbwa wanaofugwa; na pia hupenda kucheza au kuchokoza mbwa wasiowafahamu.

Alisema vimelea vya kichaa cha mbwa vinapoingia katika jeraha, hushambulia neva za fahamu kutoka katika eneo la jeraha, kuelekea katika uti wa mgongo na hatimaye kuathiri ubongo.
Serikali kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo 2030 Serikali kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo 2030 Reviewed by Zero Degree on 10/03/2019 07:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.