Loading...

Simbu akiri kuwa kuna mgogoro RT


MWANARIADHA nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu amewataka viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kuacha malumbano, sivyo mchezo huo utaendelea kuporomoka.

Akizungumza kwa njia ya mtandao kutoka Doha, Qatar jana baada ya kumaliza katika nafasi ya 16 katika mashindano ya dunia katika marathon, Simbu alisema kutofanya vizuri kwa Tanzania katika mashindano hayo kunatokana na maandalizi duni yaliyosababishwa na uongozi.

Simbu, kabla ya mbio hizo za usiku wa kuamkia jana, ndiye alikuwa mshindi wa medali ya shaba ya marathon aliyoipata baada ya kumaliza watatu katika mashindano ya dunia yaliyofanyika London 2017, lakini ameshindwa kutetea medali hiyo.

Wanariadha wengine wa Tanzania, Augustino Sulle na Stephano Huche, ambao walishiriki na Simbu marathoni hiyo ya wanaume, waliungana na Failuna aliyekimbia Septemba 27 kutomaliza mbio kutokana na joto kali.

Simbu ambaye alimaliza mbio hizo juzi kwa saa 2:13:57 alisema kuwa mwaka huu RT haikusaidia maandalizi ya timu hiyo na hiyo inatokana na mgawanyiko mkubwa uliopo ndani yake, ambao viongozi wa juu hawaelewani.

Akizungumza kwa uchungu alisema ni jambo la kusikitisha, kwani malumbano na kutoelewana kwa viongozi hao wa juu wa RT, ndiko kunachangia kwa kiasi kikubwa kuurudisha nyuma mchezo huo, ambao ulishaanza kupanda juu miaka miwili iliyopita.

Alisema kuwa kila mtu katika RT anafanya lake na timu hiyo kama waliisusa, tofauti kabisa na huko nyuma, ambapo viongozi walikuwa wamoja na walishirikiana kwa pamoja kuihudumia kambi na wachezaji wa timu ya taifa.

Simbu alisema kuwa endapo mgawanyiko huo utaendelea ndani ya shirikisho hilo, basi riadha itaendelea kutumbukia shimoni kama si kupotea kabisa.

Akizungumzia mbio hiyo ya juzi, alisema mchuano ulikuwa mkali sana na wale waliojiandaa vizuri ndio wameshinda na aliwapongeza kwa ushindi huo.

Amesema hata yeye kama angejiandaa vizuri alikuwa na nafasi ya kumaliza ndani ya tatu bora na kuondoka na medali, lakini kwa kuwa hakujiandaa vizuri, ameshindwa kumaliza katika nafasi za juu.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhlem Gidabuday, ambaye yuko Doha alipopigiwa simu hakupokea, wakati Rais wa shirikisho hilo, Antony Mtaka alipotafutwa kwa njia ya simu alisema, apigiwe baadae.
Simbu akiri kuwa kuna mgogoro RT Simbu akiri kuwa kuna mgogoro RT Reviewed by Zero Degree on 10/07/2019 01:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.