Loading...

Stars yafuzu kucheza CHAN 2020 Cameroon, yaipiga Sudani 2-1


KAMA ulivyo upepo wa kisulisuli unavyoogopeka, ndivyo ilivyokuwa kwa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuwa tishio mbele ya Sudan baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini na kufuzu michuano ya Chan ambayo inatarajiwa kufanyika Januari, mwakani nchini Cameroon.

Taifa Stars ambayo ilipoteza mchezo wa kwanza hapa nyumbani kwa kufungwa bao 1-0, jana ilihitaji ushindi wa aina yoyote ili ifuzu, ikafanikiwa kuibuka na ushindi huo kwa mabao ya beki Erasto Nyoni na mshambuliaji Ditram Nchimbi.

Katika mchezo huo wa jana uliochezwa kwenye Uwanja wa Al-Merrikh ulipo mjini Omdurman nchini Sudan, ilishuhudiwa wenyeji wakitangulia kwa bao la Amer Kamal dakika ya 30, kisha Nyoni akasawazisha kwa faulo matata dakika ya 50, kabla ya Nchimbi kufunga la pili dakika ya 79 akimalizia kazi nzuri ya Shaban Idd Chilunda.

Mashabiki kadhaa wa Taifa Stars waliojitokeza uwanjani hapa walisikika wakisema kwamba Sudan wamepitiwa na upepo wa kisulisuli, wakashindwa kujizuia na kupelekea kufungwa nyumbani kwao. Wakati dakika zikielekea ukingoni mchezo umalizike, mashabiki wa Sudan walimrushia mawe kipa wa Taifa Stars, Juma Kaseja wakati anaenda kuokota mpira hali iliyofanya mchezo kusimama kwa muda kidogo.

Hii ni mara ya pili kwa Taifa Stars kushiriki Chan michuano ambayo inahusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani baada ya awali kushiriki mwaka 2009 wakati michuano hiyo ilipofanyika nchini Ivory Coast ambapo ilipangwa Kundi A na timu za Zambia, Senegal na wenyeji Ivory Coast ambapo Taifa Stars ilimaliza nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi nne.


Ikumbukwe kuwa, hata mwaka 2009 wakati Taifa Stars imepata tiketi ya kushiriki Chan, mechi ya mwisho iliifunga Sudan nyumbani kwao mabao 2-1, baada ya mchezo wa kwanza hapa nchini Taifa Stars kushinda 3-1.
Stars yafuzu kucheza CHAN 2020 Cameroon, yaipiga Sudani 2-1 Stars yafuzu kucheza CHAN 2020 Cameroon, yaipiga Sudani 2-1 Reviewed by Zero Degree on 10/19/2019 07:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.