VAR yakataa bao la Samatta aliloifunga Liverpool, KRC Genk ikichapwa mabao 4-1
Refa huyo alikataa bao hilo lililofungwa na nahodha huyo wa KRC Genk dakika ya 26 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Junya Ito, baada ya kurudia kutazama picha za video na kujiridhisha Mtanzania huyo alikuwa ameotea wakati anafunga.
Bao hilo lingekuwa la kusawazisha baada ya Liverpool inayofundishwa na kocha Mjerumani, Jurgen Klopp, kutangulia kwa bao la nyota wa England, Alex Oxlade-Chamberlain dakika ya pili, ambaye alifunga la pili pia dakika ya 57.
Mabao mengine yote yalifungwa na washambuliaji wa Afrika, Sadio Mane kutoka Senegal dakika ya 77 na Mohamed Salah wa Misri dakika ya 87 upande wa Liverpool, huku la Genk likifungwa Mnigeria Stephen Odey dakika ya 88.
Genk inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Felice Mazzu, inabaki na pointi yake moja baada ya mechi tatu, ikifungwa mbili na kutoa sare moja, ikiendelea kushika mkia, wakati Liverpool inayofikisha pointi sita baada ya kushinda mechi moja na kufungwa moja kati ya mbili za mwanzo sasa ni ya pili Kundi E.
Mbwana Samatta akimlalamikia refa Mslovenia, Slavko Vincic jana baada ya kukataa bao lake. |
Napoli ya Italia sasa ndiyo inaongoza kundi hilo baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya wenyeji, Salzburg jana jana na kufikisha pointi saba. Salzburg inabaki na ponti zake tatu katika nafasi ya tatu.
Samatta jana amecheza mechi ya tatu Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa amefunga bao moja katika mchezo wa kwanza KRC Genk wakichapwa 6-2 na Salzburg nchini Austria.
Kwa jumla Samatta jana amecheza ya 169 kwenye mashindano yote tangu ajiunge na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 68.
Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 132 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja na Europa League mechi 24 na mabao 14.
Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa; Coucke, Maehle, Cuesta, Lucumi, Uronen, Ito, Heynen, Berge, Bongonda/Ndongalaat 66, Samatta na Onuachu/Odey dk81.
Liverpool; Alisson, Milner, Lovren, Van Dijk, Robertson/Gomez dk63, Oxlade-Chamberlain/Wijnaldum dk74, Fabinho, Keita, Salah, Firmino/Origi dk80 na Mane.
VAR yakataa bao la Samatta aliloifunga Liverpool, KRC Genk ikichapwa mabao 4-1
Reviewed by Zero Degree
on
10/24/2019 08:10:00 AM
Rating: