Loading...

Waziri Biteko atoa somo kwa wanajiolojia

Waziri wa Madini nchini Tanzania, Dotto Biteko

Waziri wa Madini nchini Tanzania, Dotto Biteko amewataka wanajiolojia wa nchi mbalimbali za Afrika kujipanga, kuangalia namna ya kuandaa miradi ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta hiyo badala ya kutegemea wahisani.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 24, 2019 katika ufunguzi wa mkutano wa wataalamu wa jiolojia ulioshirikisha wadau wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU). 

Biteko amesema kwa sasa EU ndio inafadhili miradi ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta na wanajiolojia 30 wa Tanzania wamenufaika wakati kwa bara Afrika jumla ya wanufaika ni 1,100.

"Lazima tufikirikie aina ya miradi kama hii itakayofanyika kwa nchi za Afrika, ikitokea EU wakasitisha kutoa msaada nchi hizi zimejiandaa vipi kujisimamia zenyewe namna ya kuwajengea uwezo wa ndani wanajiolojia," amesema Biteko.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Yokberth Mnyumbilwa amesema mafunzo hayo yana umuhimu kwa sababu yanaendana na shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo.

Mkuu wa Idara ya maendeleo na ushirikiano wa EU nchini, Jose Nunes amesema, “Huu ni mradi wa mfano katika kuleta mabadiliko nchini. Mafunzo yametolewa mara tano hadi sasa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Dodoma na Dar es Salaam.”

"Kupitia ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya huduma za miamba ni hatua muhimu katika kuchochea utekelezaji wa malengo ya uchumi ulimwenguni, utunzaji wa rasilimali za madini pamoja na kuendeleza sekta ya madini nchini.”
Waziri Biteko atoa somo kwa wanajiolojia Waziri Biteko atoa somo kwa wanajiolojia Reviewed by Zero Degree on 10/24/2019 08:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.