Loading...

Wanafunzi 8 mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzao



JESHI la Polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga linawashikilia wanafunzi wanane wa Shule ya Sekondari Seeke kwa tuhuma ya kumshambulia na kumjeruhi Costantine Makoye mwanafunzi mwenzao na kumsababishia majeraha ambayo yamepelekea kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Richard Abwao, amethibitisha kushikiliwa kwa wanafunzi hao na kusema kuwa tukio hilo limetokea katika Kanisa la SDA Wasabato Kahama kulikokuwa na sherehe ya kuwaaga wanafunzi wa Shirika wa Kanisa la SDA wanaotarajia kuhitimu kidato cha nne.

Kamanda Abwao amewataja wanafunzi hao wanashikiliwa kuwa ni:
  1. Isaya Athuman 18, Muha, mkazi wa Nyahanga.
  2. Godfrey Fanuel Simon, 18, Mnyiramba, mkazi wa Shunu
  3. Enock Lazaro Alfred, 17, Mhangaza, mkazi wa Shunu.
  4. Athuman Azizi, 17, Mnyamwezi, mkazi wa Shunu,
  5. Leonard Emmanuel Lutonja, 17, Msukuma, mkazi wa Shunu.
  6. Michael Philipo 17, Msukuma, mkazi wa Shunu.
  7. Sadiki Boniface Stephen, 18, Mfipa, mkazi wa Legela
  8. Emmanuel Musa Sekela, 18, Muha, mkazi wa Shunu.

Amesema baada ya sherehe kuisha katika kanisa hilo wakati wanafunzi wanatawanyika alitokea Constantine Makoye akiwa na vijana wenzie wapatao kumi ambao hawajafahamika mara moja na haijulikani kama walikuwa ni miongoni mwa waalikwa katika sherehe hiyo.

Abwao ameongeza kwamba wanafunzi hao walimvamia mwanafunzi aitwaye Isaya Athuman (18) wa kidato cha nne Sekondari ya Seeke, na kutaka kumnyang’anya viatu alivyokuwa amevaa na wengine waliwanyang’anya maji ya kunywa wanafunzi waliokuwa katika sherehe hiyo.

Ndipo wanafunzi hao walipopiga kelele na yowe kwamba wamevamiwa, ambapo waliungana na kuanza kuwarushia mawe hao waliovamia sherehe hiyo na wavamizi hao walikimbia na kutawanyika lakini Constantine Makoye alizidiwa na kulala chini na wanafunzi hao walimtelekeza hapo.

Amefafanua kuwa baadaye aliamka na kwenda nyumbani kumjulisha babu yake ambaye alimpeleka kutibiwa katika Hospitali ya Serikali Kahama bila kutoa taarifa kituoni hadi alipozidiwa tarehe 01/10/2019 akiwa hawezi kuongea, ndipo ndugu walijulisha tukio hilo kituoni na jalada lilifunguliwa kwa kosa la kujeruhi na maelekezo ya mwanafunzi huyo hayakupatikana kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Tarehe 02/10/2019 alifariki dunia wakati anaendelea na matibabu. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kubaini chanzo cha kifo ni majeraha makubwa kichwani na wamekabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokana na wanafunzi na watu waliokuwa kwenye eneo la tukio kujichukulia sheria mkononi wakimtuhumu marehemu kuwa mwizi.
Wanafunzi 8 mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzao Wanafunzi 8 mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzao Reviewed by Zero Degree on 10/07/2019 02:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.