Loading...

Ajib aahidi mambo makubwa Simba SC


MASHABIKI na wanachama wa Simba, wametakiwa kufanya kazi kwa bidii kusaka fedha, wakifahamu kuwa msimu huu wataendelea ‘kula bata’ kwani timu yao hiyo kamwe haitawapa ‘stress’.

Wito huo umetolewa na nyota wa timu hiyo, Ibrahim Ajib ambaye amesema amepania kufanya makubwa ndani ya kikosi hicho ili kuwapa raha Wanamsimbazi.

Alisema kwa kuwa wametolewa kwenye michuano ya kimataifa, akili yake yote kwa sasa ipo Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na kwamba kutokana na morali anayoiona kwa wenzake, anaamini taji la ligi hiyo litabaki Msimbazi.

Alisema mbali ya kutwaa ubingwa, wamepania kuvuna ushindi wa mabao mengi katika kila mchezo watakaocheza, ikiwa ni pamoja na kuwapa mashabiki wao burudani ‘bab kubwa’ kutokana na kundanda safi.

Kiungo mshambuliaji huyo alisema binafsi amepanga kuvuka pale alipoishia msimu uliopita alipokuwa Yanga na kufunga mabao 10 pamoja na kutoa pasi 15 za mabao (assist).

“Mipango yangu ni kuona hadi mwisho wa msimu, naipita idadi ya mabao niliyoyafunga msimu uliopita pamoja na ‘asisti’ nilizotoa na jambo hilo linawezekana.

“Ninachohitaji ni ushirikiano kutoka kwa wenzangu pamoja na mashabiki kuisapoti timu kwa sababu ligi ndio kwanza inaanza na Simba inahitaji ubingwa msimu huu,” alisema.

Alisema hivi sasa kila mchezaji anacheza kwa kujituma ili aweze kuisaidia timu kufikia malengo yake pamoja na kutimiza yale aliyoyapanga.

“Kwa uwezo wa Mungu msimu huu Simba itachukua ubingwa pamoja na mimi kutimiza yale niliyoyapanga, hivyo mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi, waendelee na majukumu yao wakifahamu kila tutakapocheza, ni ushindi tu,” alisema.

Ajib alitua Simba katika dirisha lililopita la usajili akitokea Yanga aliyoitumikia kwa misimu miwili.

Tangu ajiunge na Simba, Ajib amecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara, akianza na ile dhidi ya Kagera Sugar waliyoshinda mabao 3-0 kabla ya kuichapa mabao 2-0 Biashara United.
Ajib aahidi mambo makubwa Simba SC Ajib aahidi mambo makubwa Simba SC Reviewed by Zero Degree on 10/07/2019 02:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.