Loading...

Yanga njia nyeupe makundi CAF


WAKATI timu Yanga ikikabiliwa na mchezo wa mtoano wa kuwania kutinga makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeweka mkakati mzito kuhakikisha Wanajangwani hao wanavuka hatua hiyo.

Yanga inatarajiwa kucheza na Pyramids Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, baada ya kushindwa kutinga makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuondolewa na ZESCO United ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2.

Katika kuhakikisha Yanga inafanikiwa kuingia makundi Kombe la Shirikisho Afrika, Rais wa TFF, Wallace Karia amesema atahakikisha anakuwa bega kwa bega na timu hiyo, ili waweze kuitoa Pyramids.

Karia alisema hayo jana, wakati akizungumza na Wahariri wa Habari za Michezo kutoka vyombo mbalimbali nchini, kuelezea mafanikio aliyopata ndani ya miaka miwili tangu alipochaguliwa.

Alisema kwa kuwa imebaki timu moja ambayo ni Yanga inayoiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa, jukumu lao ni kuisaidia ili wasipoteze nafasi nne za kushiriki michuano hiyo mwakani.

Rais huyo alisema anafahamu Yanga ikitolewa hatua ya mtoano, nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa na Kombe la Afrika mwakani itabaki moja moja kwa kila michuano, badala ya mbili na kufanya kuwa na timu nne kama ilivyokuwa msimu huu.

“Sisi kama TFF tunataka kuona Yanga ikiingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ili tusipoteza nafasi nne za kushiriki michuano ya Caf mwakani,” alisema Karia.

Katika hatua nyingine, Karia alisema ndani ya miaka miwili aliyokuwapo madarakani, amepata mafanikio makubwa, yakiwamo timu za Taifa kuchukua ubingwa katika michuano mbalimbali ambazo ni Twiga Stars, Serengeti Boys na Ngorongoro Heroes.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na vipaumbele 11 alivyovitangaza kufanyia kazi kabla ya kuingia madarakani.

Karia alifanikia katika eneo la utawala bora, lakini timu ya Taifa kuzufu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2019), zilizofanyika mwaka huu, Misri ikiwa ni baada ya miaka 39.

Alisema mafanikio mengine kwa Stars ni kufuzu michuano ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi ya Ndani (CHAN), ambapo wiki iliyopita Stars ilifanikiwa kuitoa Sudan kwao baada ya kuifunga mabao 2-1.

Taifa Stars ilifuzu kutokana na ushindi wa ugenini baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Stars kufungwa bao 1-0.

Karia alisema kwa asilimia kubwa, amefanikiwa na anaendelea na maeneo mengine ya vipaumbele vyake alivyotangaza kuvifanyia kazi, ikiwamo nidhamu ya muundo wa mfumo, maendeleo ya soka la vijana, wanawake na ufukweni.

Vingine ni mafunzo ya kujenga uwezo kwa watendaji wake kuanzia ngazi za chini, kuboresha mapato na nidhamu ya fedha, maboresho katika Bodi ya Ligi, ushirikiano na wadau, udhamini na masoko, ubora wa mashindano, kuimarisha mfumo wa soka na kuimarisha sekta ya tiba na kuondoa changamoto ya waamuzi.

Chanzo: Bingwa
Yanga njia nyeupe makundi CAF Yanga njia nyeupe makundi CAF Reviewed by Zero Degree on 10/21/2019 08:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.