Loading...

55 wafariki dunia katika maporomoko ya ardhi kusini mwa Ethiopia


Watu 55 walifariki dunia Jumatatu katika maporomoko ya ardhi katika eneo la mbali la Kusini mwa Ethiopia, maafisa wa eneo hilo wamesema, wakionya kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka.

“Zaidi ya miili 55 ilipatikana kutokana na maporomoko hayo, taarifa kutoka idara ya masuala ya mawasiliano ya eneo la Gofa ilisema, ikimnuku kiongozi wa eneo hilo Dagmawi Zerihun, ambaye alionya kuwa idadi ya “vifo bado inaweza kuongezeka”.

Maporomoko hayo yalitokea saa nne asubuhi majira ya huko kufuatia mvua kubwa katika eneo lenye milima la jimbo la kusini mwa Ethiopia, Dagmawi alisema.

Wanawake na watoto ni miongoni mwa waliofariki, alisema, akiongeza kuwa shughuli za kuwatafuta manusura “zimekuwa zikiendelea”.


Picha zilizosambazwa kwenye mtandao wa Facebook na chombo cha habari kinachoshirikiana na serikali, Fana Broadcasting Corporate zilionyesha mamia ya watu karibu na eneo la tukio lililoharibika lenye udongo mwekundu ulioporomoka.

Eneo la Gofa lipo umbali wa kilomita 450 kutoka mji mkuu Addis Ababa, mwendo wa masaa 10 kwa kutumia gari.

Jimbo hilo la kusini mwa Ethiopia limeathiriwa na mvua za muda mfupi za msimu kati ya mwezi Aprili na mapema mwezi Mei ambazo zimesababisha mafuriko na watu wengi kuhama makazi yao, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya dharura ya kibinadamu (OCHA).

Chanzo: Voa
55 wafariki dunia katika maporomoko ya ardhi kusini mwa Ethiopia 55 wafariki dunia katika maporomoko ya ardhi kusini mwa Ethiopia Reviewed by Zero Degree on 7/23/2024 07:43:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.