Loading...

Mtoto aliyeibwa apatikana baada ya miezi mitano

Picha na Mtandao

Mtoto wa kike wa miezi tisa aliyeibwa katika Mtaa wa Nyihogo, Manispaa ya Kahama Desemba 9, 2023 amepatikana akiwa hai.

Imeelezwa na mamlaka za serikali kuwa mtoto huyo alipatikana Aprili 18, mwaka huu na kukabidhiwa Julai 18, mwaka huu kwa wazazi wake baada ya kuthibitishwa kwa vipimo vya vinasaba.

Mtoto huyo ambaye hivi sasa ana umri wa mwaka mmoja na miezi minne, alipatikana baada ya kutelekezwa na mwanamke aliyedaiwa kumwiba awali kwa kumlaghai dada yake kisha kutokomea naye kusikojulikana.

Baada ya kutelekezwa, aliokotwa na wasamalia wema ambao walimwona katika eneo la mtaa huo na kutoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kisisi, ambao ulimpeleka katika ofisi za Ustawi wa Jamii.

Akithibitisha kupokea mtoto huyo na kumkabidhi kwa wazazi wake, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri hiyo, Alinda Bwakea, alisema jana kuwa baada ya kuokotwa, mtoto huyo alipelekwa ofisini kwao na viongozi wa Serikali ya Mtaa kwa kufuata taratibu zote za kisheria.

Alisema kuwa baada ya kuokotwa, waliwasiliana na watu waliokuwa wametoa taarifa ya kupotea kwa mtoto na waliojitokeza walipimwa vinasaba vyao (DNA) ili kubaini kama ni mtoto wao.

Ofisa huyo alisema kuwa majibu yalitoka kuwa ni mtoto wao ambaye aliibwa na walikuwa wakimtafuta kwa kipindi chote hicho.

Bwakea alitoa wito kwa wazazi, walezi na familia nyingine kuwa makini zaidi katika suala la ulinzi wa watoto kwa wanaowalea au kucheza nao pale wanapoona mtu wasiyemfahamu - wanarubuniwa kwa kuwapatia chochote, soda na pipi zikiwa sehemu ya mtego wa wahalifu kunasa watoto.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Rose Medadi, akisimulia tukio na namna alivyoibiwa mtoto wake, alisema kuwa siku hiyo mwanawe alikuwa amebebwa na dada yake wa miaka saba wakiwa mazingira ya nyumbani, walikutana na mwizi huyo aliyewatuma wakamletee vocha dukani na kumwachia mtoto.

"Ninakumbuka maelezo ya mwanangu kuwa alitumwa vocha dukani na mama mmoja ambaye hakumtaja jina kwa kumpatia Sh. 2,000 na akamwomba ampatie mtoto kwa madai ya kuwahi na alifanya hivyo bila woga na aliporejea hakumkuta mama huyo alipomwacha," alisimulia.

Baba wa mtoto huyo, Paschal Ng’ondi alisema kuwa baada ya kufikishiwa taarifa za kuibwa mtoto wake huyo aliarifu uongozi wa serikali ya mtaa na Jeshi la Polisi na kuanza jitihada za kumtafuta.

Alisema kuwa Aprili 18 walipata taarifa za kupatikana kwa mtoto huyo na kwenda moja kwa moja ofisi za Ustawi wa Jamii.

Alisema kuwa kutokana na kumfahamu vyema mtoto wao walipofika, walimtambua ni mwanawe lakini kulihitajika kufuatwa taratibu za kisheria ikiwamo kupima vinasaba na vilipokamilika walikabidhiwa mtoto wao na wanaendelea na malezi, wakitaka wazazi wengine kuwa makini na watoto wao.

Chanzo: Nipashe
Mtoto aliyeibwa apatikana baada ya miezi mitano Mtoto aliyeibwa apatikana baada ya miezi mitano Reviewed by Zero Degree on 7/23/2024 08:12:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.