Loading...

Niliipata nafasi ya urais kama ajali - Kagame

Mgombea wa kiti cha Urais wa Chama cha FPR, Paul Kagame katika moja ya mikutano yake ya kampeni. Picha na BBC

Mwenyekiti wa Chama cha RPF Inkotanyi na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amesema kwa mara ya kwanza, nafasi ya urais aliipata kama ajali tu, huku akiwataka wote wanaouliza maswali kuhusu mrithi wake, waliache suala hilo mikononi mwa Wanyarwanda wenyewe.

Kagame anayegombea kiti cha urais kwa mara ya nne mfululizo, ameyasema hayo Jumamosi Julai 13, 2024 alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari vya ndani ya nchi hiyo.

Amesema swali hilo limekuwa likiulizwa mara kwa mara na waandishi wa habari kwenye mikutano yake ya kampeni aliyoianza takribani mwezi mmoja uliopita.

Kutokana na swali hilo, mgombea huyo, amelazimika kuelezea upya historia ya uongozi wa nchi hiyo tangu miaka 30 iliyopita.

"Kwa upande wangu kuwa rais ilianza kama ajali. Kwanza kabisa, nilinusurika na mambo mengi ambayo yangeniua, kama watu wengine wengi. Haikuwa kwa mpango. Pili, hata mwanzoni mwa mchakato huo, sikutaka kuwa rais; wale waliokuwa kwenye mamlaka wakati huo, walilazimika kumchagua mtu mwingine," Kagame amesema.

Amesema hata huyo mtu mwingine aliyechaguliwa (bila kumtaja jina), alifanya makosa na Bunge likalazimika kumwondoa na likamuomba awe mgombea naye akakubali.

“Mtu waliyemtaka wao, hakuiweza ile nafasi ya urais, Bunge likaona ni vema kumuondoa, halafu wakarudi kwangu na kunialika, nikasema sawa, hamuoni hiyo ni kama ajali tu?amehoji Kagame.

Hivyo, amesema tangu wakati huo ameendelea kuiongoza vema Rwanda na kila uchaguzi ukikaribia, waandishi wa habari na watu wengine humjia na swali hilo la anafikiria kuondoka lini.

"Tangu nilipokubali, ni kama nimefanya kosa; baadhi ya watu huniuliza nitaoondoka lini, lakini Wanyarwanda ambao nawaheshimu zaidi kuliko mtu yeyote mwingine, wanasema wanataka niendelee, lakini nawaambia hebu watafute mgombea mwingine atakayechukua nafasi hii ambaye atatembea kwenye nyayo zangu, mwaka huu hawajanipa jibu, ila nadhani mtu atapatikana hivi karibuni kwa sababu ni lazima,” amesema.

Hata hivyo, amesema jukumu la kumpata mgombea sahihi atakayekuja kuiongoza nchi hiyo si la chama cha RPF pekee, bali ni la taifa zima la Rwanda.

Lakini alitoa tahadhari kuwa jukumu la kumchagua mrithi wake si la kwake, “Nilishakiambia hata chama changu kwamba sitampendekeza mtu yeyote aje arithi nafasi hii, RPF tuko wengi, hivyo wanapaswa kukaa chini na kuchagua mtu sahihi atakayekuja kuiongoza Rwanda vizuri, hatutaki kurudi tena kwenye vita, hivyo wampate mtu kati ya watu wengi na ambaye ni sahihi,” amesema; Ameongeza: Sipendi maafa baada yangu. Waache kuchagua wanavyotaka."

Akizungumzia suala la vijana na uongozi, ametoa rai kwa vijana kuendelea kujitokeza kusaka nafasi za uongozi kwa kujiamini kwa kuwa huenda mbele ya safari akaja kupatikana rais kijana kwa kuwa muongo huu ni wa vijana kutwaa madaraka katika nyanja mbalimbali.

Amesema miaka 30 iliyopita, vijana ndiyo walisaidia kujenga misingi imara ya Rwanda ya sasa.

Alipoulizwa swali la anaionaje Rwanda baada ya kumaliza ngwe yake ya uongozi, Kagame amesema hatarajii kama itarejea kwenye machafuko, hata hivyo amesema hawezi kutabiri kitakachotokea baada yake, lakini ana imani itaendelea kuwa salama na yenye amani.

"Sina fikra kwamba kuna Kagame pekee. Kuna Kagame na watu mnawaona, tunafanya maendeleo pamoja, wananchi wanachangia sana. Mimi ninatwaa uongozi kama walivyochagua na nina hakika wakati sitakuwepo, kutakuwa na chaguo lingine ambalo linaweza kuwa bora zaidi, bila kuzingatia kwamba mambo yanaweza kutofautiana na jinsi yalivyo kuwa, lakini hivyo ndivyo maisha yalivyo,” amesema mgombea huyo.
Niliipata nafasi ya urais kama ajali - Kagame Niliipata nafasi ya urais kama ajali - Kagame Reviewed by Zero Degree on 7/15/2024 10:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.