Loading...

Rais Kagame avunja rekodi yake mwenyewe ya uchaguzi


Rais wa Rwanda Paul Kagame amevunja rekodi yake mwenyewe kwa kushinda uchaguzi wa Jumatatu kwa zaidi ya 99% ya kura, matokeo kamili ya awali yanaonyesha.

Kagame mwenye umri wa miaka 66 alishinda uchaguzi wa 2017 kwa 98.63% ya kura, kiwango cha juu zaidi ya 93% aliyopata mwaka wa 2010 na 95% mwaka wa 2003.

Wakosoaji wake wanasema ushindi mkubwa wa Bw Kagame si jambo la kushangaza kwani anatawala kwa mkono wa chuma.

Hata hivyo, wafuasi wake wanasema ushindi huo unaashiria umaarufu wake mkubwa, huku Rwanda ikiwa imepata utulivu na ukuaji wa uchumi chini ya utawala wake.

Bw Kagame ni kamanda wa zamani wa waasi ambaye majeshi yake yaliingia madarakani mwaka 1994, na kumaliza mauaji ya halaiki yaliyosababisha mauaji ya takriban watu 800,000 ndani ya siku 100.

Walipata 0.53% na 0.32% mtawalia, matokeo mabaya zaidi ikilinganishwa uchaguzi wa 2017 wakati walipataasilimia moja ya kura kwa pamoja.

Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa juu sana - 98%, kulingana na tume ya uchaguzi.

"Ushindi usio na kifani wa Kagame wa zaidi ya 99% katika uchaguzi unaashiria jinsi upinzani ulivyominywa nchini Rwanda," Clementine de Montjoye wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) alisema, katika taarifa ya AFP.

Matokeo "hayatoi picha nzuri kwa mtu yeyote anayetaka kujihusisha na shughuli halali za upinzani," aliongeza.

Lakini ushindi wa Bw Kagame ulisifiwa na Rais wa nchi jirani ya Uganda Yoweri Museveni, ambaye alisema kuchaguliwa kwake tena ni “ushahidi wa imani” waliyonayo Wanyarwanda katika uongozi wake.

Licha ya Rwanda kuendelea kukabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira kwa vijana, ni moja ya nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi barani Afrika.

Katika kampeni, Bw Kagame aliahidi kuilinda Rwanda dhidi ya "uchokozi wa nje" huku kukiwa na mvutano kati ya nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi.

Tume ya uchaguzi iliwazuia wagombea watatu wa urais, wakiwemo wakosoaji wakuu wa rais Kagame kugombea.

Iliruhusu wagombea wawili - Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party na mgombea huru Philippe Mpayimana - kugombea dhidi yake.

Chanzo: BBC
Rais Kagame avunja rekodi yake mwenyewe ya uchaguzi Rais Kagame avunja rekodi yake mwenyewe ya uchaguzi Reviewed by Zero Degree on 7/19/2024 11:08:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.