Loading...

Tumepata kambi nzuri kwa maandalizi ya msimu ujao - Dabo


Kocha wa klabu ya Azam FC, Youssouph Dabo, ameonyesha kufurahishwa na mazingira ya kambi nchini Morocco, akisema imekuwa na vitu vingi chanya ikiwemo utulivu wa wachezaji wake, vifaa vya mazoezi, viwanja bora pamoja na vyakula.

Akizungumza akiwa nchini humo ambapo kikosi cha timu hiyo kimepiga kambi kwa maandalizi ya msimu ujao wa mashindano, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara, Dabo amesema mazingira waliyoyakuta yamewafanya wao kama makocha kurahisishiwa kazi ya kuandaa kikosi bora na chenye ushindani.

"Tumepata kambi nzuri kwa maandalizi ya msimu, ni sehemu nzuri sana maana kila kitu kipo sehemu moja, ubora wa sehemu ya kuchezea ni wa viwango vya juu, vifaa vya mazoezi, hata vyakula, hii imetufanya hata makocha tusiwe na kazi kubwa sana ya kutengeneza ubora na utimamu wa mchezaji kwa sababu kila kitu kipo kwenye ubora wa hali ya juu," alisema.

Alisema kabla ya kurejea nchini watapata mechi tatu za kirafiki ambazo wao kama benchi la ufundi watazitumia kupima kikosi chao kimefikia wapi kimaandalizi na baada ya hapo wataangalia ni kitu gani cha kuongeza.

Kocha huyo pia amefurahishwa pia na usajili wa mchezaji Cheickna Diakite raia wa Mali aliyetokea klabu ya AS Real Bamako ya nchini humo.

Alisema usajili wa mchezaji huyo unataongeza ubora kwenye kikosi cha Azam FC kwa sababu anafahamu kijana huyo ana kipaji kikubwa.

"Ni mcheaji mzuri, tunampenda, tulihitaji mchezaji wa kiwango chake, huwa sichukui mchezaji ili mradi, bali mchezaji wa kutuongezea ubora, kama nitapata mwingine mzuri ninaweza kumsajili pia," alisema.

Diakite, anayecheza winga zote mbili amesajiliwa kuchukua nafasi ya Kipre Junior ambaye ametimkia MC Alger ya Algeria.
Tumepata kambi nzuri kwa maandalizi ya msimu ujao - Dabo Tumepata kambi nzuri kwa maandalizi ya msimu ujao - Dabo Reviewed by Zero Degree on 7/20/2024 06:47:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.