Lowassa: Waliomuua Mawazo wanajulikana, wakamatwe!!!
Mwanza. Mamia ya wakazi wa Mwanza na mikoa ya jirani jana walijitokeza kwa wingi kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, huku aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa akisema waliomuua mwanasiasa huyo wanajulikana na endapo polisi hawatawakamata, Chadema watachukua hatua wenyewe.
Heshima za mwisho za kuaga mwili wa Mawazo aliyeuawa Novemba 14 mkoani Geita
kwa kushambuliwa na watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CCM, zilitolewa jana katika
Uwanja wa Furahisha kuanzia saa tano asubuhi hadi saa tisa alasiri.
Utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa Mawazo ziliongozwa na Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe aliyekuwa ameambatana na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye, Lowassa na viongozi waandamizi wa chama hicho wakiwamo wabunge zaidi ya
50 wa Ukawa.
Akizungumza wakati wa kutoa salamu za rambirambi, Lowassa alisema; “Mawazo
ameuawa kinyama, polisi wasipochukua hatua kwa watu waliyofanya mauaji hayo
tutachukua hatua wenyewe.”
Aliongeza: “Imeshaelezwa kwamba wahusika wanajulikana tena kwa majina, sasa
watu hawawezi kusubiri haki kama wanaona vyombo husika vya kutenda haki
vinashindwa kufanya kazi yao.”
Akizungumzia tukio la kuzuiwa kuaga mwili huo hadi kwa amri ya Mahakama,
Lowassa alisema kinachofanywa na polisi ni kutafuta uhalali wa kutumia fedha za
wananchi walizozitumia kununua silaha ambazo zilishindwa kufanya kazi wakati wa
uchaguzi.
“Hapa kulitolewa sababu za kipindupindu ili watu wasiage mwili wa Mawazo,
lakini sababu hizo zilikuwa ni uongo mtupu.. hakuna cha kipindupindu wala nini.
Mahakama imetenda haki, hata Biblia inasema waacheni watu wazike wafu wao,
uamuzi wa Mahakama Kuu itakuwa somo kwa nchi nzima, mimi nampongeza jaji
aliyeruhusu watu kumuaga Mawazo,” alisema Lowassa.
Wakati Lowassa akisema hayo, Sumaye alisema haki isipopatikana kwa amani
itapatikana kwa njia nyingine, huku akitoa mfano wa askari wa makaburu
walivyowakandamiza watu wa Afrika Kusini, lakini walipoamua kutafuta haki
walifanikiwa kuwatoa.
“Mimi ni mgumu sana kutoa machozi, hata baba yangu alipofariki sikutoa
machozi, lakini leo nimetoa machozi kwa sababu nchi ambayo ilikuwa na misingi ya
amani, leo tunashuhudia watu wanaodai haki wanauawa, ni jambo la kusikitisha,”
alisema Sumaye.
Aliwataka waombolezaji wasimamie amani lakini wasikubali kuonewa, kwa kuwa ni
lazima wapinge dhuluma.
Mkumbo mahakamani
Akihitimisha kutoa salamu za rambirambi, Mbowe alisema watampeleka Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo mahakamani ili ajue gharama za kuwaweka
Mwanza mawaziri wakuu wastaafu; Lowassa na Sumaye pamoja na wabunge 50 wa Ukawa
na kuwafanya wananchi watumie siku 14 kuomboleza msiba, asubiri samansi,”
alisema Mbowe.
Mbowe alisema walipopata taarifa za Mkumbo kuzuia mwili wa Mawazo usiagwe
mkoani hapa, walishtuka kuona polisi wanazuia haki ya kikatiba na kibinadamu kwa
madai kwamba makazi ya marehemu yalikuwa mkoani Geita.
“Nilitamani kumuona Mawazo bungeni, kwani naamini alikuwa ni sawa na zaidi ya
wabunge 20 wa CCM, nilitamani kumwona Wenje akizungumza bungeni,” alisema Mbowe
na kuongeza:
“Najua watu wengi watajiuliza kwa nini Mawazo, lakini ifahamike kuwa Mawazo
alitoa maisha yake yote kufanya kazi za ukombozi, tena bure, hakuwa mwajiriwa wa
Chadema, mtajiuliza kwa nini tumekuja kuweka kambi Mwanza, lakini ni vyema kila
mtu afahamu Mungu alipenda msiba wa Mawazo ufanyike hivi ili ufumbue macho ya
Watanzania kwamba baadhi ya polisi hawatendi haki.”
Katika hatua nyingine, Mbowe alitaja baadhi ya majina ya watu waliopoteza
maisha wakati wa kupigania haki, kuwa ni pamoja na mwandishi wa habari, Daudi
Mwangosi, Ali Zona wa Morogoro na waandamanaji watano waliopoteza maisha mkoani
Arusha.
Chadema na familia ya Mawazo
Akizungumzia jinsi Chadema itakavyoshirikiana na familia ya marehemu, Mbowe
alisema mpaka sasa ana majina ya watu watatu waliyojitolea kumsomesha mtoto wa
marehemu, Precious Mawazo, akiwamo Lowassa na kwamba wameamua wabunge 113 wa
Ukawa kila mmoja achange Sh300,000 ili kupata Sh33.9 milioni zitakazowekwa
kwenye mfuko wa maalumu utakaoisaidia familia hiyo.
Baadaye, Mbowe alimkaribisha jukwaani aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana, Ezekia
Wenje azungumze na waombolezaji na alipofika alisema anajua kuwa watu wana
majonzi ya kumpoteza Mawazo pamoja na kuibiwa kura, lakini amekwenda mahakamani
na anasubiri uamuzi mwingine.
“Najua mna majonzi mengi, mmeibiwa kura, tumempoteza Mawazo, ila kila kitu
kina makusudi yake. Haki huwa inacheleweshwa tu, lakini inapatikana kwa
yaliyotokea yamenifanya niwe jasiri zaidi,” alisema Wenje.
Mtoto wa marehemu awaliza waombolezaji
Akitoa neno kwa waombolezaji, mtoto wa marehemu, Precious ambaye ana umri wa
miaka tisa alisema yeye na mdogo wake ambaye ana miaka miwili wanaitaka Serikali
ikomeshe mauaji ya namna hiyo.
“Baba yetu ameuawa kinyama, naamini damu yake itasimama kwa kila mtu
aliyepanga mauaji yake, najua ameuawa akipigania haki na mimi naamini siku moja
nitafuata nyayo zake na kuwa mwanasiasa mkubwa,” alisema Presious huku
akibubujikwa na machozi.
Lema amlilia Mawazo
Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema hakutarajia kama
angemzika Mawazo akiwa chini ya miaka 40 na kwamba yeye ndiye aliyemuingiza
kwenye siasa.
“Nimeumizwa na kifo cha rafiki yangu wa damu Mawazo, mimi ndiye
niliyemuingiza kwenye siasa hata alivyokuja Arusha alikuwa anaishi nyumbani
kwangu na familia yake. Nilimshauri aje Mwanza na baadaye Geita, kwa kweli kifo
chake kimeniuma na cha kusikitisha mwili wake umeteseka,” alisema Lema na
kuongeza;
“Polisi isifanye mzaha na damu za watu, Mawazo ameuawa akipigania haki...
Nasikitika kuona tunafanyiwa maigizo kwenye hili, siku moja watu wakichoka
magari yenu hayatafanya kazi.”
Mahubiri.
Katika mahubiri yake, Mchunganji wa Kanisa la Winners Mwanza, Bernard Swai
alisema damu ya Mawazo bado inalia mbele za Mungu na akaitaka Serikali
ihakikishe kila aliyehusika anatiwa nguvuni.
“Serikali ihakikishe inawakamata waliohusika ili wachukuliwe hatua, kama
isipowakamata, Mungu mwenyewe atajua cha kufanya na hawataishi kamwe,” alisema
Swai.
Baba mdogo wa marehemu, Mchungaji Charles Rugiko aliishukuru Mahakama kwa
kutenda haki na kuongeza kwamba, “Mawazo hajafa, ila waliomuua ndiyo wamekufa,
kwani damu yake bado inalia mbele za Mungu.”
Mwili wa Mawazo ulisafilishwa jana kwenda mkoani Geita kwa ajili ya mazishi
yatakayofanyika kesho kjijini kwao, Butundwe.
Mshirikishe na mwenzako!!!
Mshirikishe na mwenzako!!!
Lowassa: Waliomuua Mawazo wanajulikana, wakamatwe!!!
Reviewed by Zero Degree
on
11/29/2015 10:42:00 AM
Rating: