Hizi hapa athari nyingine za unywaji pombe kupitita kipimo.
Maeneo mengi nchini hususani miji mikubwa, pombe imekuwa ikinywewa kwa wingi, hususani kwa vijana kuanzia umri wa miaka 15 na kuendelea.
Mbaya zaidi pombe zimekuwa zikiuzwa si tu kwenye baa na klabu lakini saa hata kwenye maduka ya vyakula ambayo biashara ya pombe kali aina ya kiroba imeshamiri kwa kasi, kitu kinachoonyesha wazi kuwa biashara hii ina faida kubwa na wanywaji wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku, kitendo ambacho hata bajeti ya Serikali kwa miaka mingi imekuwa ikitegemea kwenye bajeti.
Pamoja na Taifa kutegemea pato lake kutoka kwenye pombe, bidhaa hii imekuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa hali ya ustawi wa afya ya mwili wa mwanadamu, hususani kiakili.
Tunapozungumzia afya tunamaanisha hali ya ustawi wa mwanadamu kimwili, kiakili na kijamii.
Mtu mwenye afya njema ya akili anaaminika kutengemaa katika namna anavyofikiri, anavyohisi, na anavyotambua mambo, ambayo kwa pamoja hujionyesha katika matendo yake ya kila siku.
Pombe na magonjwa ya akili
Magonjwa ya akili yanaathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, na hivyo kuwa na tabia au mwenendo uliotofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, desturi, na nyanja nyingine za kijamii.
Tabia hizo zinatokana na ugonjwa wa akili kuathiri ufanisi na shughuli za mtu husika (mgonjwa) au huathiri jamii nzima inayomzunguka endapo mgonjwa huyo hatapatiwa matibabu stahiki na kwa wakati mwafaka.
Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina idadi ya watu takriban milioni 45 na kutokana na taarifa ya afya ya akili kwa mwaka 2014/15 inaonyesha kuwa idadi ya watu 817,532 wanaugua magonjwa mbalimbali ya akili nchini, hii ni karibu asilimia 2 ya Watanzania wote.
Pia idadi hii ni ongezeko la wagonjwa 367,532 ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2013/14 walikuwa ni 450,000.
Kati ya wagonjwa wote wa akili kwa mwaka 2014/15 wanawake ni ni 332,000 na wanaume ni 485,532. Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi nchini ukifuatiwa na mikoa ya Lindi na Dodoma.
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili, Praxeda Swai anasema asilimia 20 ya wagonjwa wa akili na saikolojia hutumia kilevi, huku asilimia 50 hadi 75 ya watumiaji wa pombe wapo hatarini kupata magonjwa ya akili.
Anasema kuna ugonjwa wa akili unaotokana na mambo mengi ikiwamo utumiaji wa pombe, dawa za kulevya, kuna asilimia 3.3 vya vifo vinatokana na unywaji pombe, huku kundi kubwa likiwa ni vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 25.
Dalili ya kichaa
Dk Swai anasema kuna vichaa vya aina nyingi, vikiwamo vya kimwili na kiakili.
Kichaa cha kimwili dalili zake anazitaja kuwa ni kukosa nguvu au kuhisi mwili una nguvu sana kupita kiasi, kukosa usingizi au kulala kupita kiasi, kukosa hamu ya kula au kuwa na hamu ya kula
Nyingine ni kutotulia (kuhamanika) au kutulia sehemu moja muda mrefu bila ya kujisogeza, maumivu sehemu za mwili kama vile kichwa, mabega, mgongo na viungo ambavyo mgonjwa akienda hospitali vipimo havionyeshi tatizo lolote la kimwili.
Anasema dalili za kichaa cha akili ni pamoja na kukosa umakini wa shughuli zake za kila siku, kusahau haraka au kupoteza kumbukumbu, kukosa uwezo wa kupambanua mambo kwa mitazamo tofauti, kusikia sauti ambazo hazipo na kuona vitu ambavyo havipo, imani ya ajabu ambazo haziendani na mila, imani au desturi za jamii yake.
Pia anaamini ana nguvu ya ziada kutoka nje ya mwili inayomsababishia kutenda au kuwaza mambo anayoyawaza. Mawazo yake hayana mtiririko unaoeleweka.
Baadhi ya aina za magonjwa ya akili ni kama vile magonjwa ya kuchanganyikiwa, magonjwa yanayohusiana na matumizi mabaya ya pombe na utumiaji wa dawa za kulevya. Pia magonjwa ya wasiwasi au hofu na woga, magonjwa yanayoathiri hisia ambayo husababisha watu kujiua na matatizo ya jinsia.
Magonjwa haya mara nyingi yanapoanza yanaonekana ni hali ya kawaida tu na huenda pasiwapo na jitihada yoyote ya kupata msaada wa kitabibu hadi hali inakuwa mbaya na kuzidiwa na hapo ndiyo mtu analipuka kichaa sugu.
Pombe husababisha saratani
Dk Swai anasema unywaji pombe hausababishi kichaa peke yake, bali pia saratani ya mahali popote katika mwili hususani kwenye mfumo wa chakula, huku ini likiathiriwa zaidi.
Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya akili anatanabahisha kuwa pombe imekuwa ikipunguza nguvu za uzazi kwa wanaume na wanawake, huku wanaume wakiwa kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na tatizo hilo kwani mbegu zao huathirika kutokana na matumizi ya pombe kwa asilimia 72.
Pombe imechangia kwa kiasi kikubwa kusambaratika kwa familia kutokana na unyanyasaji unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na unywaji pombe, huku watoto wakiathirika zaidi ikiwamo kutelekezwa.
Kifafa cha mimba
“Kifafa cha mimba asilimia 100 kinachangiwa na unywaji pombe kipindi cha ujauzito, hata watoto wanaozaliwa wanakuwa kwenye athari ya kuwa mazezeta, ‘’ anasema.
Source: Mwananchi
Hizi hapa athari nyingine za unywaji pombe kupitita kipimo.
Reviewed by Zero Degree
on
1/29/2016 05:02:00 PM
Rating: