Loading...

Kipindupindu CHAZIDI kushika kasi hapa Nchini.


Ugonjwa wa Kipindupindu katika wiki iliyopita umeongezeka kutoka wagonjwa 138 walioripotiwa kuanzia Mei Mosi mwaka huu hadi 9 na kufikia 212; Nsachris Mwamwaja ambaye ni Afisa Habari wa Wizara ya Afya kwa niaba ya Dk. Ummy Mwalimu ambaye ni Waziri wa Wizara hiyo amesema idadi ya vifo pia imeongezeka.

“Takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2016 zinaonesha kuwa kasi ya ugonjwa imeongezeka kidogo ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa wiki hiyo ni 212 ikilinganishwa na 138 walioripotiwa wiki iliyotangulia (Mei, 2 hadi 8, 2016),” amesema Mwamwaja.

Aidha, idadi ya vifo vitokanavyo na kipindupindu pia imeongezeka katika wiki hiyo ambapo viliripotiwa vifo vitano ikilinganishwa na vifo viwili vya wiki iliyotangulia.

“Wiki iliyoanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2016, jumla ya mikoa minane imeripoti Ugonjwa wa Kipindupindu. Mikoa hiyo ni Morogoro (78), Lindi (51), Manyara (42), Dar es Salaam (16), Mara (8), Pwani (8), Kilimanjaro (6) na Kagera (3),” amesema Mwamwaja.

Amesema Mikoa minne kati ya hiyo iliripoti vifo vilivyotokana na ugonjwa wa kipindupindu; Lindi (2), Morogoro (1), Mara (1) na Kagera (1).

Aidha Wizara imesema hadi kufikia Mei 15 mwaka huu, jumla ya wagonjwa 21,477 wametolewa taarifa, na kati ya hao 338 wamepoteza maisha ambapo wizara imeendelea kuisisitiza jamii kujenga na kutumia vyoo bora ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo kwa kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.




ZeroDegree.
Kipindupindu CHAZIDI kushika kasi hapa Nchini. Kipindupindu CHAZIDI kushika kasi hapa Nchini. Reviewed by Zero Degree on 5/17/2016 10:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.