Loading...

Polisi wafanikiwa kuua jambazi mmoja kati ya watatu walioshiriki kupora fedha jijini Dar.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, KamishnaSimon Sirro.

Dar es Salaam. Matukio ya uhalifu yameendelea kulitikisa jiji la Dar es Salaam baada ya polisi kumuua mtu mmoja anayesadikiwa kuwa jambazi, kati ya watatu waliopora fedha eneo la Buguruni Chama. 

Kabla ya kuuawa jana saa sita mchana, watu watatu walimpora mtu aliyekuwa kwenye gari aina ya Toyota IST, lililokuwa kwenye foleni Barabara ya Mandela kwa kuvunja kioo cha mbele kwa jiwe.

Polisi walisema majambazi mawili walitoweka na wanaendelea kusakwa na kwamba, kiwango cha fedha zilizoibwa hakijafahamika.

Mashuhuda wa tukio hilo, walisema mtu huyo ambaye jina lake halijafahamika alikuwa ndani ya gari lake lililokuwa kwenye foleni ya kwenda Tazara, ghafla majambazi watatu waliokuwa wamepakizana kwenye bodaboda walishuka na kumgongea kioo kabla ya kufanya uporaji.

Mmoja wa mashuhuda hao, Juma Abdallah alisema baada ya kulifuata gari hilo, majambazi hao walimuamuru dereva ashushe kioo na awape haraka begi linalodaiwa lilikuwa na fedha.

“Dereva alikuwa peke yake na alikuwa mbishi kutii amri ya majambazi hao. Baada ya kuona hali imekuwa ngumu, jambazi moja alitoa bastola na kupiga tairi la mbele kuzuia gari lisiondoke,” alisema Abdallah na kuongeza:

“Hata hivyo, dereva alizidi kuwawekea ngumu licha ya mbinu zote walizotumia, lakini mwishowe jambazi mwingine aliamua kuokota jiwe na kuvunja kioo na kutoa begi lenye fedha.”

Baada ya kutoa begi, alisema walitoa fedha zilizokuwamo na kulitupa chini begi hilo kisha kupanda bodaboda waliyokuwa wameiegesha umbali wa mita kama tano kutoka eneo la tukio.

Kuona hivyo, wakazi wa eneo hilo walianza kuwarushia mawe majambazi hao huku waendesha bodaboda wakiwafukuza kuelekea Ubungo.

Mwendesha bodaboda wa Tabata Matumbi, Hamis Jumaa ambaye pia alishuhudia tukio hilo, alisema aliona pikipiki hiyo ikiwa mwendokasi ikifukazana na raia na polisi, ghafla walikatisha kuelekea Kigogo.

“Tuliamua kuungana na wenzetu katika msafara huo lakini tulipofika Matumbi Gereji karibu na benki moja hivi, jambazi mmoja alitoa bastola kupiga moja ya pikipiki na kumjeruhi bodaboda mmoja,” alisema Jumaa.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema katika tukio hilo walikamata bastola mbili na kwamba, jambazi aliyepoteza maisha alifariki dunia akipelekwa hospitali.

Hata hivyo, Kamishna Sirro hakuwa tayari kutaja kiwango cha fedha kilichoporwa badala yake alisisitiza polisi wanaendelea na upelelezi na kwamba kesho watatoa taarifa rasmi.




ZeroDegree.
Polisi wafanikiwa kuua jambazi mmoja kati ya watatu walioshiriki kupora fedha jijini Dar. Polisi wafanikiwa kuua jambazi mmoja kati ya watatu walioshiriki kupora fedha jijini Dar. Reviewed by Zero Degree on 5/29/2016 09:59:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.