Loading...

Benki zatekeleza AGIZO lililotolewa na Makonda.


WAKATI siku 21 zilizotolewa kwa benki zilizokuwa zikitumika kuweka mishahara ya watumishi hewa zikiwa zimeisha jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema ameshapata taarifa alizohitaji kutoka katika benki hizo.

Makonda alisema benki hizo zimeshapeleka taarifa ingawa aliahidi kutoa ufafanuzi zaidi baada ya kukaa na kuzipitia. Makonda alitoa siku hizo 21 zilizoisha jana, benki hizo kurejesha fedha hizo serikalini au zitaje watu waliokuwa wakitumia akaunti husika.

Alichukua hatua hiyo baada ya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa na ongezeko kubwa la watumishi hewa ambao fedha walizokuwa wanalipwa zilikuwa zinapita katika benki husika. Mpaka sasa, mkoa wa Dar es Salaam umebainika kuwa na watumishi hewa 283, ambao wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 3.6 ambazo zilitumika kuwalipa mishahara.

Makonda alisema benki ndio pekee wanaoweza kusaidia mkoa, kutambua wahusika waliokuwa wanatumia akaunti hizo pamoja na wale waliokuwa wanachukua fedha hizo.

Alitaja benki hizo na fedha zilizoko ni NMB yenye Sh bilioni mbili, CRDB zaidi ya Sh milioni 400, NBC zaidi ya Sh milioni 141, DCB Sh milioni 85, Standard Chartered zaidi ya Sh milioni mbili na Community Benki zaidi ya Sh milioni 100.

“Hakuna mtu anayeweza kutumia akaunti ya mtu bila kufuata taratibu za kibenki, hata kama mtu amefariki kuna taratibu za kufuata ndipo apate akaunti, naamini benki hizi zitasaidia kuwatambua wahusika wote,” alisisitiza.


ZeroDegree.
Benki zatekeleza AGIZO lililotolewa na Makonda. Benki zatekeleza AGIZO lililotolewa na Makonda. Reviewed by Zero Degree on 6/15/2016 10:17:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.