Loading...

Makonda kuzawadia bendi zawadi ya shilingi milioni 1/=

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa tatu kushoto) akiwa na wanamuziki wa bendi mbalimbali za muziki wa dansi nchini ofisini kwake jana.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameahidi kutoa zawadi ya Sh milioni 1 kwa bendi itakayofanya vizuri kwenye Tamasha la bendi mbalimbali za muziki wa dansi linalotarajiwa kufanyika leo kwenye viwanja vya Leader Club Kinondoni.

Ahadi hiyo aliitoa mbele ya wanamuziki hao wa dansi waliokwenda ofisini kwake kumtaarifu adhima ya tamasha hilo, ambalo sehemu ya mapato yake yatatumika kuchangia madawati.

“Najua nyimbo za dansi zinatoa ujumbe mzuri wenye kuelimisha tofauti na hizi za muziki wa kizazi kipya, ambao mara nyingi wanaimba mapenzi naahidi bendi itakayotoa burudani nzuri nitaipa zawadi ya milioni moja”, alisema Makonda na kushangiliwa na wanamuziki hao.

Pia Makonda alisema anatarajia kuwapo pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kupata burudani kwani si kila muda mafaili tu.

Naye Ally Choki akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema wanatarajia kutoa burudani kali kwa mashabiki kwani muziki utapigwa ‘live’.

“Tamasha hili ni la kwanza Tanzania na linatoa fursa kwa wanamuziki wa dansi wakongwe na chipukizi kukutana kwenye jukwaa moja hali ambayo itajenga umoja na kikubwa kuchangia madawati ili kuboresha elimu kwa watoto wetu, “ alisema Choki.

Bendi zitakazotumbuiza kwenye tamasha hilo ambalo limeandaliwa na Kampuni ya Tanzania Band Festival ni Msondo Ngoma Musica Band, Mlimani Park Orchestra,The African Stars Band, FM Academia, Mapacha Watatu, Ya Moto Band, B Band ya Banana Zorro, Top Band ya TID, Skylight, La Capitale ya King Kiki na bendi nyingine nyingi. Kiingilio ni 15,000 na tamasha litaanza saa tano asubuhi na kumalizika usiku wa manane.

ZeroDegree.
Makonda kuzawadia bendi zawadi ya shilingi milioni 1/= Makonda kuzawadia bendi zawadi ya shilingi milioni 1/= Reviewed by Zero Degree on 7/29/2016 10:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.