Loading...

Pluijm: Mambo yamekuwa magumu.

KOCHA wa Yanga, Hans van Pluijm amekiri kuwa mambo yamekuwa magumu kwa upande wao katika michuano ya hatua ya makundi ya Kombe la Shrikisho Afrika na kwamba wanarudi kujipanga upya kwa ajili ya mwakani.

Yanga ilikubali kipigo cha mabao 3-1 mbele ya wapinzani wao, Medeama ya Ghana juzi ukiwa ni mchezo wa nne wa michuano hiyo na kuiacha timu hiyo ikiendelea kuburuza mkia huku ikiwa imebakiwa na mechi mbili kabla ya kumalizika kwa hatua hiyo ya makundi.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao, Pluijm alisema matokeo hayo yamewapa funzo kubwa na kama kocha analazimika kukitathmini upya kikosi chake kabla ya kuelekea kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

“Tuliingia uwanjani tukiwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi hasa ukizingatia huo ndiyo mchezo uliokuwa umebeba matumaini yetu ya kufika kule tulipopataka, lakini baada ya nusu saa mambo yakawa tofauti na kubwa ni uzoefu wa wachezaji wangu hasa wale wa nafasi ya ulinzi hawakucheza kwa kiwango chao,” alisema Pluijm.

Mholanzi huyo alisema ukiacha makosa ya walinzi wake, kwa ujumla wachezaji wake walicheza chini ya kiwango na kuwapa nafasi wenyeji wao Medeama kufanya wanavyotaka na kufunga mabao hayo ya haraka ambayo alikiri yalichangia kuwatoa mchezoni.

Alisema kukosekana kwa beki raia wa Togo, Viccent Bossou nako kulichangia wao kupoteza mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao kutokana na uzoefu aliokuwa nao kwenye michuano mikubwa kama hiyo, lakini atahakikisha wanarudi kujipanga ili kumalizia mechi zao mbili zilizobaki ambazo amepania kuhakikisha wanashinda.

Matokeo hayo yamepoteza kabisa matumaini ya kocha Pluijm kuiona Yanga ikicheza nusu fainali ya michuano hiyo kwa mwaka huu, baada ya kupata pointi moja katika michezo minne waliyocheza huku wakifungwa mechi tatu na kutoka sare mchezo mmoja na sasa wanahitaji miujiza ili kufuzu hatua hiyo ya nusu fainali.

ZeroDegree.
Pluijm: Mambo yamekuwa magumu.  Pluijm: Mambo yamekuwa magumu. Reviewed by Zero Degree on 7/28/2016 12:23:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.