Loading...

Siku ya mashujaa yahamishiwa Dodoma.

RAIS John Magufuli ameonesha nia ya kuhamia Dodoma kwa kuanza kushughulikia masuala muhimu, ikiwamo ya kuzindua awamu ya kwanza ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma na kuhamishia maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mkoani hapa.

Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa kitaifa wa amani ulioandaliwa na Jumuiya ya Ahamadiyya, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema katika kuonesha dhamira ya kuhamia Dodoma ambao ulitangazwa kuwa Makao Makuu ya Tanzania miaka ya 1970, Rais alielekeza fedha zilizobaki kwenye bajeti iliyopita zitumike kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege ambao pia ujenzi wake utazinduliwa na Rais mwenyewe Julai 22, mwaka huu.

Aidha, Rugimbana alisema Rais Magufuli pia ameagiza maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mwaka huu yahamie Dodoma ambapo kwa miaka mingi sasa yamekuwa ikifanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa, Mnazi Mmoja Dar es Salaam.

“Ndio natoka kwenye kikao cha kuzungumzia maadhimisho hayo kufanyika Dodoma hilo linadhihirisha wazi dhamira ya Rais kuhamia Dodoma,” alisema Rugimbana na kuongeza kuwa Rais Magufuli atashiriki Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) utakaoanza Julai 23, mwaka huu.

Akizungumzia suala la amani, mkuu huyo wa mkoa alisema serikali itawachukulia hatua kali viongozi wa taasisi mbalimbali ambao wamekuwa na tabia za kutumia nafasi zao kuhubiri uchochezi na hivyo kutishia amani na utulivu wa nchi.

Alisema viongozi ambao wamekuwa na tabia za kutumia taasisi zao kama sehemu ya kuhubiri masuala ya uovu, ikiwemo kushawishi vitendo vya uvunjifu wa amani, serikali haitawafumbia macho.

Aliwataka viongozi wa dini nchini kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba za taasisi zao na siyo kufanya mambo kwa maslahi yao binafsi na tamaa. Alisema pia serikali inaunga mkono jitihada za taasisi za dini katika kuhubiri amani na utulivu wa nchi ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi mbalimbali.

“Kama serikali, tunaunga makono jitihada zenu mbalimbali ikiwemo kupinga vitendo vya maovu pamoja na ufisadi ambao umekuwa ukilitafuna taifa letu,” alisema.


ZeroDegree.
Siku ya mashujaa yahamishiwa Dodoma. Siku ya mashujaa yahamishiwa Dodoma. Reviewed by Zero Degree on 7/15/2016 11:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.