Loading...

Yanga kamili kushuka dimbani kesho dhidi ya wenyeji wao Medeama nchini Ghana.

YANGA iko kamili na kesho itaendelea na hesabu za kujaribu kujichomoa kutoka kwenye wakati mgumu michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wawakilishi hao wa Tanzania, watakuwa wageni wa Medeama ya Ghana katika mchezo wa marudiano ya michuano hiyo.

Akieleza jinsi mipango yake itakavyokuwa kwenye mchezo huo, Kocha Hans van der Pluijm alisema wanakwenda kusaka pointi tatu ugenini ili kujiweka kwenye mazingira mazuri Kundi A la michuano hiyo.

Alisema pamoja na kutambua kuwa wanacheza ugenini, hawataubeba mfumo wa kujiami kwa kupaki basi, badala yake mkazo mkubwa utakuwa kushambulia mfululizo.

Alisema makosa yaliyofanywa na wachezaji wake, hasa safu ya ushambuliaji kupoteza nafasi nyingi za kufunga, hategemee tena kuyaona kwenye mchezo huo.

"Hii ni mechi muhimu sana kwetu, matokeo yoyote ambayo hayatatupa pointi tatu, maana yake tunakwenda kujiweka kwenye wakati mgumu," alisema Pluijm.

Yanga inakwenda kuwavaa wenyeji wao wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare mchezo wa kwanza baada ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Wawakilishi hao wa Tanzania wana pointi moja na bao moja, baada ya sare moja na kufungwa mbili. Wanaburuza mkia kwenye kundi lao linaloongozwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Salehe alisema wachezaji wote wako kwenye hali nzuri na kwamba hakuna majeruhi.

"Kikubwa mwalimu amesisitiza umakini muda wote wa mchezo. Tunashukuru wachezaji wapo katika hali nzuri na wanatambua umuhimu wa kushinda mchezo huo," alisema Hafidhi.

Alisema timu ilifanya mazoezi jana jioni tayari kwa mchezo huo.

"Mwalimu ameshafanya kazi yake kwa asilimia kubwa, sasa kazi imebaki kwa wachezaji ndani ya uwanja.Tunategemea watatimiza yale waliyofundishwa na mwalimu.

Wakati Yanga wakitarajiwa kucheza kesho, TP Mazembe wenyewe watawakaribisha Mo Bejaia mjini Lubumbashi. Mchezo wao wa kwaza uliochezwa nchini Algeria, timu hizo hazikufungana.


ZeroDegree.
Yanga kamili kushuka dimbani kesho dhidi ya wenyeji wao Medeama nchini Ghana. Yanga kamili kushuka dimbani kesho dhidi ya wenyeji wao Medeama nchini Ghana. Reviewed by Zero Degree on 7/25/2016 10:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.