Loading...

Waziri aanika jinsi kina Lissu walivyomtesa.

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum akifanyiwa mahojiano maalumu na mwandishi wa gazeti la nipashe rahma suleiman visiwani zanzibar.
ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, amekiri kuwa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, kamwe hatalisahau katika maisha yake ya uongozi kwa sababu lilimkosesha usingizi kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza wakati akihojiwa na Nipashe juzi, Waziri huyo alisema kilichokuwa kikimkosesha amani zaidi katika sula hilo, ni ukweli kwamba wabunge walichachamaa mno bungeni huku yeye akiwa ndiyo kwanza amepewa kuongoza wizara hiyo kwa cheo cha uwaziri na masuala yote yanayohusiana na akaunti hiyo yalifanyika kitambo kirefu kabla ya kuteuliwa kwake.

Mkuya alifichua ukweli huo wakati akijibu swali lililomtaka ataje mambo mawili mazuri na yaliyompa changamoto kubwa kiasi cha kutikiswa wakati akiiongoza Wizara ya Fedha.

“Wakati nateuliwa kuwa Waziri wa Fedha, ni wakati ule ule ambao sakata la Escrow lilipokuja juu. Kila mtu alitafsiri vyake, kwa hiyo sakata la Escrow halikunipa amani hata kidogo,” alisema Mkuya na kuongeza:

“Mimi nilikuwa katika hiyo nafasi wakati huo, lakini mchakato (wa akaunti ya Tegeta Escrow) ulikamilika wakati sipo. Kwa hiyo haukunipa amani mpaka zilipochukuliwa hatua.”

Miongoni mwa wabunge waliokuwa mstari wa mbele kuibana serikali bungeni kuhusiana na sakata la Akunti ya Tegeta Escrow ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR-Mageuzi, David Kafulila; aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) ambaye sasa ni kiongozi wa ACT-Wazalendo anayewakilisha Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe; Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee na Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora.

Wabunge wengine waliokuwa moto bungeni wakati wa sakata hilo ni aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro ambaye sasa ni msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka; aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) ambaye sasa ni Mbunge wa Bunda kwa tiketi ya Chadema, Esther Bulaya na aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (CUF) ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Kaliua kupitia chama hicho, Magdalena Sakaya.

Kwa nyakati tofauti, wabunge hao na wengine karibu wote, kutoka kambi ya upinzani na pia chama tawala, CCM, walisimama kidete kuhakikisha kwamba serikali inatoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na kashfa hiyo itokanayo na utata kuhusu mitambo ya kufua umeme ya IPTL iliyoko Tegeta jijini Dar es Salaam.

Mkuya alisema alikosa amani kwa muda wote kuhusiana na sakata la Escrow na wabunge walivyokuwa wakichachamaa hadi pale maazimio ya Bunge yalipofikiwa, ingawa nayo yalikuwa na changamoto nyingine ya kuhitaji mchakato wa kisheria kuyatekeleza.

“Maazimio hayo yalikuwa yakihitaji mchakato wa kisheria zaidi. Kwa hiyo, ni kitu ambacho hakikunipa amani hata siku moja katika kipindi kile,” alisema Mkuya.

Miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa bungeni kuhusu Escrow yalisababisha kukosa uwaziri kwa Prof. Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na pia aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Prof. Sospter Muhongo.

Hivi sasa, Muhongo aliyerejea bungeni baada ya kushinda katika uchaguzi uliopitia alikogombea katika Jimbo la Musoma Vijijini (CCM), amerudi katika nafasi hiyo baada ya kuteuliwa na Rais wa Serikali ya awamu ya tano, John Magufuli.

Kabla ya kuteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kushika nafasi ya uwaziri wa fedha, Mkuya alikuwa akishikilia nafasi ya unaibu waziri katika wizara hiyo wakati wa uongozi wa Dk. William Mgimwa (sasa marehemu).

Mkuya ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Jimbo la Welezo visiwani Zanzibar, kwa mara ya kwanza aliteuliwa na Kikwete kuwa Mbunge kupitia nafasi 10 za rais kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha.

Alipandishwa cheo na kuwa waziri kamili katika wizara hiyo mwaka 2014 baada ya kufariki kwa Waziri Mgimwa.

MAHOJIANO

SWALI 1. Nani alikuvutia hadi ukajitosa katika masuala ya siasa?
SAADA MKUYA: Awali, mimi nilikuwa mtaalamu katika Wizara ya Fedha na nilikua nikiipenda kazi yangu. Na masuala ya siasa hayakua katika moyo wangu, na wala hakuna mtu aliyekuwa akinishawishi… lakini nilikuwa napenda kufuatilia siasa za kimataifa… na mimi kuingia katika siasa kuna watu waliona uwezo wangu kwa sababu mimi niliteuliwa ubunge kupitia nafasi 10 za rais.

SWALI: Baada ya kushinda ubunge wa jimbo la Welezo na pia kuwahi kushika nafasi ya juu kiuongozi ya uwaziri wa fedha katika Serikali iliyopita, nini kilichobaki katika ndoto zako kwenye medani za siasa? Kwamba, labda siku moja utajitosa katika mbio za urais… maana bado waonekana u-kijana sana mheshimiwa…

SAADA MKUYA: Ubunge niliteuliwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2012. Nikawa mbunge… baadaye nikawa Naibu Waziri wa Fedha na kisha nikawa Waziri wa Wizara ya Fedha.

Na sasa hivi ni Mbunge wa Jimbo lakini ndoto ninazo za kuwa kiongozi wa juu zaidi na inawezekana, tena kwa nafasi za kimataifa zaidi.

Nikipata hiyo nafasi… kwa sababu sasa hivi nafanya PhD, naamini kuwa ni mwanamke ambaye nitawakilisha vyema taifa katika medani za kimataifa.

SWALI: Ulipokuwa Waziri, ni mambo gani makubwa uliwahi kukumbana nayo katika utendaji wako na kamwe hutayasahau? … kwa uchache tukumbushe walau mawili mazuri na mawili yaliyojaa changamoto kiasi cha kukutikisa…

SAADA MKUYA: Ni mambo mengi. Kwa sababu ukiwa katika wizara ya fedha unakuwa katika kiti ambacho matukio ya kila wakati ya nchi yanakuhusu kwa namna moja ama nyingine… kwa hiyo cheo cha Wizara ya Fedha ni kikubwa na hakikupi muda wa kupumzika.

Sasa kubwa langu mimi ni wakati nateuliwa kuwa Waziri wa Fedha… ni wakati ule ule ambao sakata la Escrow lilipokuja juu.

Kila mtu alitafsiri vyake. Kwa hiyo sakata la Escrow halikunipa amani hata kidogo… lakini jambo jingine ni ukusanyaji wa mapato.

Wakati tunaingia sisi, ilikuwa lazima tulete mabadiliko ya njia za kuweza kukusanya mapato. Wafanyabiashara walijipanga kushindana na Serikali kuona kuwa hawawezi kutumia EFD (mashine za kielektroniki).

Kwa hiyo ugumu wake ulikuja kwa sababu katika ile nafasi ya uwaziri, ni mimi imenibidi nisimame na kupigania katika kuhakikisha Serikali inapata mapato yake yanayostahili na kuweza kutekeleza bajeti… ilikuwa na ugumu wake kwa sababu Waziri wa Fedha nilikuwa peke yangu na jambo kama hujapata ushirikiano na wengine haliwezi kusimama.

Kwa hiyo nilikuwa napigana vita ambayo naweza kusema kuwa (sasa) napata ahueni kwa sababu Serikali nzima iko katika mwamko wa matumizi ya huduma ya kielektroniki … ni vitu vingi lakini pengine vitu vikubwa ni hivyo viwili ambavyo vilikuwa vikiniumiza kichwa.

SWALI: Inakumbukwa ulipambana vilivyo ukishirikiana na wasaidizi wako kuweka mambo sawa wakati wa sakata la Escrow… tueleze ni kipi cha ziada ulijifunza, hasa bungeni kuhusiana na sakata lile lililokuwa gumzo nchini kote?

SAADA MKUYA: Mambo ni mengi ya kujifunza lakini kiukweli naweza kusema funzo kuu ambalo nimepata ni kwamba kwa namna yoyote, ukiwa katika nafasi ya uongozi lazima ufanye kazi ya ziada kuhakikisha lolote unalolifanya linakwenda kwa kufuata aratibu na sheria.

Ni bora uchelewe kuliko kuraharakisha. Kwanza lazima miongozo ya nchi na sheria na taratibu zake zifuatwe katika utekelezaji wa jambo lolote.

Kwa hiyo, hilo ni funzo kubwa. Lakini jambo jingine nililojifunza (ni kwamba) inawezekana mtu au kikundi cha watu kinaweza kutengeneza jambo kama wamekukusudia tu mtu fulani lazima tumng’oe, wanaweza kutengeneza hilo jambo na usiwe na nafasi ya kujitetea… ya kueleza ukweli au hata ukieleza ukweli unaweza ukapindishwa huo ukweli ili kuhakikisha kwamba matakwa ya watu ambao wanataka jambo lao lifanikiwe na wakaweza kufanikiwa… lakini jambo la tatu nililojifunza ambalo ndiyo kubwa zaidi, ni la kujifunza kwamba vyombo vya habari vina nafasi kubwa sana ya kuweza kubadilisha maono ya wananchi.

Kwa ninachozungumza katika chombo cha habari, wananchi wanasikiliza na wanaweza kutambua kama kuna ukweli wowote.

Lakini kubwa zaidi, kama chombo cha habari, tunaweza tukasema kuwa kimejikita… wananchi wanakuwa na maono chanya kwenye suala zima la maendeleo… kwa hiyo chombo cha habari kina nafasi kubwa katika kuendeleza maendeleo ya nchi.

SWALI: Kuna kina mama wengi huhofia kwenda kugombea ubunge kwa kuhisi kwamba watashindwa kutokana na mfumo dume na matokeo yake huishia kuwania viti maalumu. Kipi kilikupa ujasiri hadi ukajitosa Jimbo la Welezo na mwishowe kushinda?

SAADA MKUYA: Kwanza wakati mimi naingia Bungeni, unajua kwamba kule Bungeni kuna maono tofauti kama mwanamke wa viti maalumu, kwamba kidogo kuwa katumia nyenzo ambazo zipo chini kidogo ukilinganisha na jimbo.

Hata kule Bungeni huwa wanakushangaa ukishinda jimboni… watu wengi wanaweza kukushangaa, lakini kwangu mimi, labda inatokea na mazingira yenyewe.

Kugombea viti maalumu kunakuwa na watu wachache wa kuweza kuwashawishi wakupigie kura ukilinganisha na jimboni.

Lakini uelewa wangu mimi, kwenda kugombea jimboni maana yake kila mahala uende, kila kichochoro upite, kila mtu umuone ili umshawishi aweze kukupigia kura… kwa hiyo maono yanakuwa tofauti na ukitoka unaonekana kuwa mpambanaji… lakini mimi nadhani jambo jingine inaweza ikawa ni maono lakini siyo… inaweza ikawa sio sahihi.

Lakini kwangu mimi, nilikuwa na maamuzi mbalimbali kuwa naenda viti maalumu lakini mwisho wa siku nikasema wacha niende jimboni … unaweza watu wakakuona na kukufahamu na wakaweza kukuunga mkono.

Kwa hiyo mimi wito wangu mkubwa, hata mwanamke ukiamua kwenda jimbo nenda tu jimboni na kushindwa haimaanishi kuwa umeshindwa kila kitu… na siyo lazima kuwa mbunge… unaweza kuwa mtu mwingine kutokana na uzoefu ulioupata wakati ukigombea ubunge kupitia jimbo.

Kwa hiyo wanawake wajitokeze, waende wakagombee jimboni… hivyo vizingiti kama na sisi tutavipalilia basi vitakuwapo lakini kama tutakuwa sisi ni wa kwanza kuviondosha, kweli vitaweza kuondoka.

SWALI: Una lipi la kuwaeleza wanawake wengine na hasa vijana wakiwamo wa Zanzibar kuhusiana na ushiriki wao katika chaguzi?

SAADA MKUYA:
Kwanza vijana wana nafasi kubwa ya kubadilisha mfumo mzima wa uongozi. Kwa hiyo, kikubwa vijana kwanza wajikite katika kushiriki kuwania nafasi kwenye uchaguzi…. na wao waweze kuwa na mwamko kushiriki katika kuchagua kiongozi ambaye wanahisi atawafaa, atawaletea maendeleo.

Changamoto zipo nyingi zinazowakabili vijana. Ajira hakuna, lakini watafute mtu ambaye wanahisi kuwa ataweza kuwaletea maendeleo na baada ya uchaguzi lazima wawe wanasimamia kwa yule ambaye waliyomchagua afanye kile ambacho aliwaahidi. Kwa hiyo wana nafasi kubwa kuendeleza nchi.

SWALI: Hali ya Zanzibar kisiasa inaelezewa kuwa inapita katika kipindi kigumu kutokana na mgawanyiko wa kiitikadi miongoni mwa wananchi ambao wengi ni CCM na CUF… inadaiwa wengine hawazikani wala kuoana kwa sababu hiyo. Je, una lipi la kuzungumza kuhusiana na hilo?

SAADA MKUYA: Ni kweli tunakoelekea siyo kuzuri sana.

Jambo kama hilo limenitokea jimboni kwangu, siyo kwenda kuzikana lakini kulikuwa na tatizo la kisima… yaani kuna baadhi ya kikundi cha upinzani walikuwa wanasema kuwa kuna kisima kilichimbwa na Mbunge wa CUF, kwa hiyo wakawa wanawakataza wafuasi wa CCM wasitumie maji hayo.

Lakini kwa kushirikiana na Serikali kupitia Mkuu wa Wilaya na Mkoa, tumeweza kulitatua jambo hilo. Unajua ni jambo ambalo watu wanataka elimu kuwa siasa kuziweka kando na kuingia katika mustakbali wa kimaendeleo… lakini leo hii unamnyima binadamu maji unakuaje? Kwa hiyo, siasa tuzipe nafasi zake kama siasa lakini tushirikiane katika kuhakikisha ustawi wa wananchi na maisha yao yanaimarika.

Vinginevyo tunaweza kujikuta kama wenzetu ambao sasa wanaitafuta amani. Mungu atunusuru tusifike huko.

SWALI: Nini kifanyike ili kuondokana na mgawanyiko huo?

SAADA MKUYA: Kikubwa wananchi waelimishwe athari ya mgawanyiko uliopo. Kwamba tusigawanyike kwenye misingi ya kisiasa kwa sababu siasa tunaweza tukasema ni itikadi zetu za kidunia, lakini tuangalie sana.

Umoja na mashirikiano ndiyo dira ya maendeleo.

Lazima tusaidiane. Kwa mfano, mimi ni Mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi, lakini naamini kwamba kuna watu ambao walikuwa siyo wanachama wa CCM lakini walinipigia kura kwa hiyo nina wajibu sasa kuwaweka pamoja na kuwaletea maendeleo kwa pamoja kwani maendeleo hayaji kwa mtu mmoja mmoja.

Kwa hiyo tuangalie la mbele zaidi kwani kipindi cha siasa kimeshapita na tusubiri mwaka 2020 kuanza mchakato mwingine wa kisiasa.

SWALI: Hivi sasa makusanyo ya kodi yameongezeka hadi kuvuka trilioni moja kwa mwezi baada ya serikali kuchukua hatua kadhaa ikiwamo kupambana vilivyo na ukwepaji wa kodi bandarini na kwingineko…unadhani ni kipi kiliwakwamisha wakati wewe ukiwa waziri hadi kodi ikaonekana kuwa chini ya trilioni moja kwa mwezi wakati wenu?

SAADA MKUYA: Wakati mimi nikiwa Waziri… kwanza nafurahi kuwa maelekezo mengi ambayo tuliyokuwa tumeyaweka yamekuwa yakitekelezwa sasa hivi.

Kwa hiyo naweza kusema ule msingi tumeuweka sisi. Lakini watu wakumbuke kuwa mimi nilikaa uwaziri wa fedha kwa muda wa mwaka mmoja na nusu kuanzia Februari 2014 hadi Oktoba 2015.

Lakini najua kuwa tumeleta mabadiliko mengi ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi, tumeweza kutengeneza mifumo ya ukusanyaji wa kodi kwa njia za kieletroniki, ambacho sasa hivi ndiyo kinachofanyika na mapato yamefikia hivyo. Lakini vile vile tumepambana sana.

Mimi mwenyewe binafsi, nikiwa waziri nilikuwa nikitembea bandarini na niliona kabisa kwa macho yangu kuwa watu wanapitisha bidhaa huku kile kinachoandikwa katika fomu sicho ambacho kinaletwa serikalini.

Mimi mwenyewe nimekwenda na nimeona… nafurahi kuwa sasa hivi hata mwenyewe Rais na Waziri Mkuu wanakwenda na wanakiona.

Kwa hiyo… ilikuwa ni udhibiti kwanza… unaanza kutatua tatizo halafu unafanya udhibiti. Kwa hiyo sisi wakati wa kipindi chetu hatukufikia huko lakini tulikuwa na malengo ya kufikia huko.

Tulikuwa tumefikia bilioni mia nane na mia tisa, lakini nyuma ya hapo fedha hizo zilikuwa hazipatikani.

Tulikuwa tunaona hasa kuwa hapa tukisimamia udhibiti na utendaji tunaweza tukafikia katika trilioni moja na zaidi. Na tuliweka misingi mizuri ambayo inatekelezwa sasa hivi.

SWALI: Na je, una lipi la kumuusia waziri aliyepo sasa na wananchi kwa ujumla katika kuhakikisha kuwa mapato ya nchi yanaongezeka maradufu?

SAADA MKUYA: Kwanza nampongeza kwa kazi nzuri anayoifanya. Lakini kimsingi kuwepo na taratibu zaidi za usimamizi na udhibiti wa ulipaji wa kodi. Kwamba kila mtu awe anawajibika kulipa kodi, Kwa hiyo usimamizi unahitajika.

Hata hivyo, waziri anatakiwa kila mara awe anatoa taarifa kwa wananchi ili kuwaelimisha wajibu wa kulipa kodi ni wajibu wa kila mtu.

Sasa kama wewe mwananchi unalipaje kodi yako? Ni kwamba ukienda dukani unataka kununua kitu dai risiti na ukidai risiti utakuwa umejihakikishia kwamba kodi yako ambayo ulistahiki kulipia basi unalipa na humfaidishi mfanyabiashara… kipindi chetu sisi ni jambo ambalo hata mwananchi hakuelewi.

Mimi nilishawahi kwenda dukani mtu anapewa risiti… na muuza duka alikuwa akinijua mimi ni nani. Kwa hiyo alikuwa na hofu akatoa risiti.

Lakini kwa kuwa yule mwananchi aliyenunua bidhaa alikuwa hanijui mimi ni nani akasema kuwa risiti sina haja nayo, Kumbe elimu ilikuwa tunaielekeza kwa wafanyabiashara…. kumbe sasa elimu inapaswa ielekezwe zaidi kwa wananchi ambao ndiyo wengi wanaonunua bidhaa.

Pia waziri aliyepo asisahau kwamba Wizara ya Fedha ni Wizara ambayo inaunganisha pande mbili za Muungano wa Tanzania… kwamba ahakikishe maslahi ya Zanzibar yanasimamiwa na kutekelezwa.

Lakini kuna fursa ambazo Zanzibar lazima iwepo, lazima ahakikishe kuwa Zanzibar inashiriki katika fursa mbalimbali ambazo zinakuja kwa jina la Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikubwa mapato ambayo yanastahiki kuja Zanzibar yahakikishwe kuwa yanasimamiwa kwa ajili ya kutengeneza bajeti ya Serikali ya Zanzibar.

Kwa hiyo mambo ni mengi… kwa sababu mapato ndiyo msingi mkuu aone umuhimu wa kuweza kuwa na uwiano kuwa mapato ya Zanzibar yanakuja Zanzibar lakini vilevile kuwashajihisha wananchi wawe wanalipia kodi wanavyostahiki kwa kupitia kudai risiti na wafanya biashara kutoa risiti za kieletroniki.

SWALI: Kama una jingine lolote la kuongeza Mheshimiwa.

SAADA MKUYA: Maendeleo ni mchakato. Lakini tunahitaji kwenda kwa nguvu zaidi… wananchi wajue kuwa tunaanza na moja, tunakwenda na nyingine… na mtazamo wangu zaidi utakwenda kwa jimbo langu la Welezo.

Wasione kwamba tumechaguliwa tukiwa na miezi minane halafu anakuja mtu anasema anataka maji katika bomba… hapana.

Rasilimali zipo chache, inabidi tuzigawanye katika umeme, maji na barabara kwa sababu kuna baadhi ya maeneo katika jimbo langu hata umeme hayana.

Kwa hiyo mahitaji yapo mengi lakini rasilimali ni chache… kwa hiyo wakumbuke kuwa tunawajali, tunajua matatizo yaliyopo na sisi tupo kazini katika kuhakikisha tunaondosha hayo matatizo ambayo yapo.
Lakini kwa upande mwengine, wanawake wasiogope kuingia katika uongozi.

Kwamba kama mwanamke umeweza ukabeba mimba na ukaweza kumlea mwanao mpaka pengine mwanao yupo chuo kikuu au anafanya kazi, basi ujuwe umefanya kazi kubwa sana… uone kama mwanamke ameweza kufanya hayo basi mwanamke hawezi kushindwa sehemu yoyote.

Hata kuiongoza nchi anaweza… kwa hivyo tusiogope, tuingie katika ushindani, katika kinyang’nyiro ili sisi tuchangie kuondosha mfumo dume huu ambao upo…mfumo dume huu utaondoshwa na sisi wanawake na wala siyo wanaume.

Utaondoshwa na sisi wanawake katika kuingia katika michakato ya kugombea nafasi za uongozi na kisha tukipata nafasi za uongozi kwenda mbele kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo.


Credits: Nipashe
ZeroDegree.
Waziri aanika jinsi kina Lissu walivyomtesa. Waziri aanika jinsi kina Lissu walivyomtesa. Reviewed by Zero Degree on 8/14/2016 08:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.