Loading...

Rais Magufuli atoa siku 7 kwa wadeni wa Shirika la Nyumba la Taifa [ NHC ].

Rais John Magufuli akizungumza na waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota alipokutana nao, Dar es Salaam jana.
RAIS John Magufuli ametoa siku saba kwa taasisi zote za serikali zinazodaiwa malimbikizo ya kodi na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha zinalipa madeni yao, vinginevyo mali zao zitatolewa nje.

Dk Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Nehemia Mchechu kutomuogopa mtu yeyote awe Rais, Waziri, CCM, Chadema au kiongozi yeyote wa serikali endapo hajalipa pango lake la nyumba, atolewe nje mali zake.

Pamoja na hayo, mkuu wa nchi amewaahidi wakazi 644 wa eneo la Magomeni Kota, Kinondoni, Dar es Salaam kuwa ndani ya miezi miwili ujenzi wa nyumba za kisasa utaanza katika eneo hilo, na ndani ya mwaka mmoja ukishakamilika, wakazi hao watakuwa wa kwanza kupatiwa nyumba hizo.

Akizungumza na wazee waliokuwa wakazi wa eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema tayari ameshatoa maagizo kwa taasisi zozote za serikali ikiwemo wizara zinazodaiwa na NHC, kuhakikisha zinakamilisha kulipa madeni yao ndani ya siku saba.

“Wasipolipa nakuagiza bwana Mchechu watolee nje mali zao kama ulivyomtolea nje yule jamaa. Usiogope mtoe mtu yeyote asiyelipa pango hata kama ni serikali, waziri, Ukawa, Rais au CCM. Lazima watu hawa wakulipe ili upate fedha za kuliendesha shirika hili,” alisisitiza Rais Magufuli.

Aliwataka wapangaji wote wa shirika hilo kuhakikisha wanalipa fedha za pango la nyumba na endapo wapo ambao hawajalipa wajiandae kuondoka kwenye nyumba hizo.

“Nashangaa eti hawa wa serikalini wanashindwa kulipa pango la nyumba kwa NHC, lakini fedha za safari za nje wanazo kila kukicha, wanaomba vibali vya kusafiri na kulipana posho,” alisema na kuongeza kuwa endapo shirika hilo litazitolea nje baadhi ya taasisi na wizara za serikali kwa kushindwa kulipa kodi, itakuwa ni vyema kwa kuwa sasa taasisi hizo zitaenda moja kwa moja Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kikamilifu.

Hivi karibuni, Mchechu alitoa mwezi mmoja kwa kampuni 29 za taasisi mbalimbali za serikali zilizokwepa kulipa madeni yake kwa shirika hilo la nyumba la Taifa.

Miongoni mwa taasisi hizo zinazoongoza kudaiwa na NHC madeni ambayo yamefikia zaidi ya Sh bilioni tisa ni pamoja na Ofisi ya Rais inadaiwa zaidi ya Sh milioni 10 na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inadaiwa zaidi ya Sh bilioni mbili.

Taasisi nyingine ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni moja; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inadaiwa zaidi ya Sh bilioni moja; Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inadaiwa Sh milioni 613 na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inadaiwa Sh milioni 360.

Mchechu alisema pamoja na deni hilo, wapo taasisi na watu binafsi akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ambaye hivi karibuni mali zake zilitolewa nje kwa kushindwa kulipa deni lake.

Mbowe anayeendesha Club Bilicanas iliyoko maeneo ya Posta, Dar es Salaam anadaiwa zaidi ya Sh bilioni 1.1.

Awali akizungumzia mgogoro wa ardhi katika eneo la Magomeni Kota, Dk Magufuli aliwatoa machozi wakazi wa eneo hilo baada ya kuwaahidi kuwatimizia makubaliano yao waliyoingia na halmashauri ya manispaa ya Kinondoni miaka mitano iliyopita.

Alisema ahadi ya ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo hilo, itaanza kutekelezwa ndani ya miezi miwili na ujenzi wa nyumba hizo utakamilika ndani ya mwaka mmoja ambapo wakazi hao 644 watapatiwa nyumba za kuishi watakazoishi kwa muda wa miaka mitano bure.

“Kwanza nawaomba radhi kwa usumbufu mkubwa mliopitia, haingii akilini muondolewe kwenye nyumba zenu kwa ahadi ya kujengewa nyumba mpya na kulipwa pango, bila kutimiziwa. Mlinichagua mimi Magufuli kuwa Rais wenu, sasa nasema kuanzia sasa mateso kwenu tena basi,” alisema.

Alisema wakazi hao waliotaabika kufuatilia haki yao mahakamani kwa muda wa miaka mitano tangu mwaka 2012 walipotolewa kwenye nyumba hizo, watapatiwa nyumba hizo za kisasa kulingana na taarifa zao na orodha ya majina yao ambayo Rais huyo anayo.

Alisema eneo hilo la ekari 33 sasa litajengwa nyumba hizo za kisasa yakiwemo maghorofa, ofisi na maeneo ya biashara kadri atakavyoshauriana na NHC na Wakala wa Majengo (TBA).

Kauli hiyo ya Magufuli iliamsha shangwe na vilio vya furaha miongoni mwa wakazi hao waliokusanyika katika mkutano huo, ili kujua hatma yao huku wengine, wakimuombea kwa sauti Rais huyo wakitaka Mungu amlinde azidi kutetea wanyonge.

“Naenda kupanga mikakati, nitatoa fedha za serikali mwezi huu ili mkandarasi atakayepatikana aanze kujenga nyumba hizi. Wakati wakiendelea kujenga nyumba hizi, maeneo mengine pia nayo yataendelea kujengwa ili kuendeleza zaidi eneo hili,” alisisitiza.

Alisema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa jiji la kisasa la kibiashara ambalo wakazi wake wote wanakuwa na makazi bora bila kujali kipato chao.

Aidha, Rais Magufuli alisema aliamua kumteua Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli kuongoza manispaa hiyo ili apambane na vitendo vichafu vya uonevu wa ardhi na kudhibiti wale matajiri wanaotaka kuchukua maeneo ya wazi kwa faida zao binafsi.

“Hali ilikuwa mbaya, ndio maana watu walitaka kujimilikisha hadi fukwe, walibakisha kidogo tu wajiuzie ikulu. Nimechagua viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa makusudi kabisa, ninataka mabadiliko ya kweli katika jiji hili,” alifafanua.

Naye Msemaji wa Wakazi wa Magomeni Kota, Mchungaji John Raymond alisema wakazi hao walikubaliana na Manispaa ya Kinondoni, wapishe ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo hilo tangu mwaka 2012 na baada ya ujenzi huo kukamilika watapangishwa na kuuziwa nyumba hizo.

Aidha, alisema pia walikubaliana katika kipindi chote ambacho ujenzi huo unaendelea, manispaa hiyo iliahidi kuwalipa wakazi hao pango la nyumba, ahadi ambayo hadi sasa haijatimizwa na hivyo kusababisha wakazi hao kuidai manispaa hiyo kiasi cha Sh milioni 4.3 kila mmoja.

Alisema kwa niaba ya wakazi hao wanamuomba Dk Magufuli serikali iwajengee nyumba wakazi hao za bei nafuu, kwani kitendo cha kuondolewa kwao kwenye nyumba za kota bila malipo yoyote kimesababisha vifo vya wazee 15 baada ya kupatwa na shinikizo la damu.

Naye Mwenyekiti wa Wazee wa Magomeni Kota, Mwajuma Sama, aliangua kilio mbele ya Rais wakati akitoa shukurani kutokana na uamuzi wa kiongozi huyo wa kuwapatia nyumba za kisasa wakazi hao na kuwapa muda wa miaka mitano kukaa bure kwenye nyumba hizo.

“Mungu akulinde baba, tumetolewa kwenye nyumba hizi nikiwa na miaka 64, leo nina miaka 70 napata matumaini. Nakuombea Mungu akusimamie baba uishi miaka mingi,” alisema mwanamama huyo, huku akilia kwa sauti hali iliyozua vilio pia kwa akinamama wenzake waliokuwepo kwenye mkutano huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alikiri kuwa mgogoro huo ni muda mrefu kwani nyumba hizo zilikuwa chini ya Serikali za Mitaa na bvaadaye NHC lakini kutokana na kushindwa kuziendeleza kama ilivyokubaliwa ardhi hiyo ilirejeshwa serikali kuu.

“Na nyumba zote alizoniagiza Rais Magufuli zenye migogoro ya aina hii nimeshaandaa tangazo la serikali (GN) zote zitarejeshwa kwanza kwa serikali kuu,” alisema.

Alisema tangu awe waziri wa ardhi, ameshuhudia migogoro mingi ya ardhi na mingi ikitokana na ufisadi wa maofisa ardhi hali iliyosababisha apime viwanja 600 maalumu kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wote waliodhulumiwa ardhi na maofisa hao.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliwashukia wale wote wanaomkashifu Dk Magufuli kwa kumuita dikteta kutokana na maamuzi anayoyatoa na kusisitiza maamuzi yote ya Rais huyo yamelenga kuondoa kero za wanyonge.

Alisema tangu Rais huyo atangaze kuijenga barabara ya Mwenge-Morocco, kuagiza ndege mpya za Serikali na ujenzi wa mahakama ya mafisadi, kumekuwa na madai mengi ya kumvunja moyo, hali ambayo wananchi wanapaswa kutoiunga mkono.

“Mheshimiwa Rais unaposikia mawimbi na dhoruba zinapiga mchana usiku ujue Mungu hajalala, itafikia wakati wasaidizi wako nikiwemo mimi tutakukimbia utabaki mwenyewe, usikate tamaa jua Mungu hajalala. Rais anapochukua uamuzi wa kurejesha eneo kwa wanyonge kuna watu tu hawatafurahia hatua hii,” alisema.

Credits: Habari Leo
ZeroDegree.
Rais Magufuli atoa siku 7 kwa wadeni wa Shirika la Nyumba la Taifa [ NHC ]. Rais Magufuli atoa siku 7 kwa wadeni wa Shirika la Nyumba la Taifa [ NHC ]. Reviewed by Zero Degree on 9/07/2016 07:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.