Loading...

Posho za Mwenge zafutwa, ..Rais aagiza waliokwishalipwa wazirejeshe.

RAIS John Magufuli ameagiza viongozi wote wa serikali, walioalikwa kuhudhuria sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, zitakazofanyika kesho katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, kutohudhuria sherehe hizo.

Pia, ameagiza wale ambao walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo, wazirejeshe.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu jana ikimkariri Katibu Mkuu Kiongozi Balozi, John Kijazi, ilieleza kuwa Rais Magufuli ametoa maagizo hayo, ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.

Waliofutiwa safari Viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni wakuu wote wa mikoa, wakuu wote wa wilaya, wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, mameya na wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.

“Kwa kuwa sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka viongozi wote wa mikoa na wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo,” ilieleza taarifa ya Ikulu.

Iliongeza kuwa Rais Magufuli ameagiza wilaya zote zilizofanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha mbio za Mwenge. Kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.

“Hata hivyo, Dk Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo, wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016,” iliongeza taarifa hiyo ya Ikulu.

Aidha, ilisema mgeni rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru, atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.

Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli alitangaza kuwa serikali yake itabana matumizi yasiyo ya lazima, ikiwamo kuondoa posho mbalimbali pamoja na kufuta safari zisizo na lazima za ndani na nje ya nchi, huku akielekeza fedha nyingi katika kuhudumia wananchi.

Mchumi alonga

Akizungumzia uamuzi huo wa Rais Magufuli, Mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Lenny Kasoga alisema uamuzi huo ni sahihi, ingawa kuna sherehe zinatumia fedha zaidi ya kuingiza.


ZeroDegree.
Posho za Mwenge zafutwa, ..Rais aagiza waliokwishalipwa wazirejeshe. Posho za Mwenge zafutwa, ..Rais aagiza waliokwishalipwa wazirejeshe. Reviewed by Zero Degree on 10/13/2016 08:48:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.