Loading...

Rais Magufuli afanya ziara ya kushtukiza uwanja wa ndege mara baada ya kumuaga Rais Kabila, ..atumbua maofisa wawili waliomdanganya.

RAIS John Magufuli amefanya ukaguzi wa kushitukiza katika sehemu ya kukagulia mizigo na abiria ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam upande wa Terminal One na kuagiza maofisa wawili, waliotoa taarifa za uongo kwake Mei mwaka huu, wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Mei mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza mara baada ya kuwasili kwenye uwanja huo akitokea jijini Kampala nchini Uganda, ambako alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Museveni. Alitembelea kwa kushitukiza na kubaini kuwa mashine za ukaguzi (scanners) zilikuwa hazifanyi kazi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu akikagua mashine ya ukaguzi wa mizigo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Terminal One kuangalia ufanisi wa mashine hizo.

Lakini jana baada ya kumsindikiza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye alikuwa akiondoka nchini baada ya ziara ya siku tatu, aliamua kufanya tena ukaguzi wa kushitukiza, na mara hii amebaini kuwa mashine hizo zinafanya kazi, baada ya kujionea yeye mwenyewe uhalisia wa namna mizigo inavyokaguliwa.

Hata hivyo, amemuagiza Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Paul Rwegasha kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa wawili waliotoa taarifa za uongo alipofanya ukaguzi wa kushitukiza mara ya kwanza.

“Leo kweli mashine zinafanya kazi na mimi nimeona, lakini wale walionidanganya mara ya kwanza nilipokuja, mkurugenzi hakikisha unawachukulia hatua,” alisisitiza Dk Magufuli, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana.

Rais Magufuli aliagiza maofisa hao, ambao kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ni Lilian Minja na Novia Maduka ambao ni maofisa oparesheni wa JNIA, washushwe vyeo.

Alipofanya ziara ya kushitukiza kwa mara ya kwanza Mei 13, mwaka huu, Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi ya dosari za ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria Terminal One.

Aliitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa mashine za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na mizigo hazifanyi kazi kwa muda mrefu.

Maofisa wa uwanja huo waliokuwa wakitoa maelezo juu ya hali ya kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria kwenye uwanja huo, walikuwa wakitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu utendaji kazi wa mashine za ukaguzi, hali iliyosababisha Rais Magufuli aamue kuiagiza wizara husika kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja.

“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri uzungumze ukweli tu, kwa nini nimeanzia hapa huwezi ukajiuliza?

Eeeh sasa sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa hivi, wewe umenidanganya kwamba hiyo ndio mbovu na hii ndio nzima, nikawaambia muiwashe hiyo nzima, akaja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii ni mbovu kwa miezi miwili,” Rais Magufuli aliwahoji maofisa wa uwanja wa JNIA wakati huo.

ZeroDegree.
Rais Magufuli afanya ziara ya kushtukiza uwanja wa ndege mara baada ya kumuaga Rais Kabila, ..atumbua maofisa wawili waliomdanganya. Rais Magufuli afanya ziara ya kushtukiza uwanja wa ndege mara baada ya kumuaga Rais Kabila, ..atumbua maofisa wawili waliomdanganya. Reviewed by Zero Degree on 10/06/2016 08:39:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.