Loading...

Utata mamilioni ya Prof. Lipumba

Baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba, kuamua kukiendesha chama hicho kwa fedha zake za mfukoni.

Haijajulikana mara moja Profesa Lipumba anakopata fedha hizo, lakini yeye mwenyewe amekuwa akiwaambia watu wake wa karibu kuwa ni malipo yanayotokana na kazi zake za kushauri masuala ya uchumi katika ngazi ya kimataifa.


Taarifa za uhakika na ambazo gazeti hili limezinasa, zinaeleza kuwa hata ziara aliyoifanya hivi karibuni katika baadhi ya mikoa ikiwamo Lindi na Mtwara, imefanikishwa kwa mamilioni ya fedha zilizotoka katika mfuko wa Prof. Lipumba.

Aliporejeshwa tu katika nafasi yake ya uenyekiti na Jaji Francis Mutungi, ambaye ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Lipumba alikaririwa akisema alikuta akaunti ya chama hicho ikiwa haina senti hata moja.

Hata hivyo, alisema suala la fedha ndani ya chama hicho linasimamiwa na Bodi ya Wadhamini wa chama pamoja na Katibu Mkuu, Maalim Seif, ambaye anatambuliwa kama ‘mhasibu mkuu’.

Mbali na taarifa hizo, madai mengine yaliibuka hivi karibuni yakimtuhumu Profesa Lipumba kufungua akaunti benki kwa lengo la kuingiziwa fedha za ruzuku, jambo lililopingwa vikali na Baraza la Wadhamini, likisema ni kinyume cha sheria na kwamba mkakati huo una taswira ya kuwavuruga.

Taarifa za sasa za kiongozi huyo kutoa fedha zake mfukoni, zimethibitishwa pia na msaidizi wake wa karibu, Abdul Kambaya, ambaye anashikilia wadhifa wa Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa chama hicho.

Kambaya ambaye anatajwa kama msiri mkubwa wa Prof Lipumba, alikiri kiongozi huyo kutumia fedha zake za mfukoni, akisema amelenga kutekeleza dhamira yake ya kutibu majeraha yaliyotokana na msuguano uliopo kati yake na baadhi ya viongozi wa chama chao.

Alitoa ufafanuzi huo baada ya gazeti moja hapa nchini siku ya Jumapili kuhoji chanzo cha fedha zilizowezesha ziara ya kisiasa ya Prof. Lipumba aliyoifanya hivi karibuni.

Akizungumza kwa sauti ya ukali kidogo, Kambaya alisema bajeti ya ziara ya Prof. Lipumba katika mikoa hiyo ilikuwa ni shilingi milioni tatu, kiasi ambacho si rahisi kwa mwenyekiti huyo kushindwa kukimudu.

“Ah! Wanaohoji Profesa Lipumba kutoa fedha CUF ni wajinga tu, kwani mara ngapi Profesa kakisaidia chama? Kwani wakati chama kinafanya kampeni mwaka 1995 wakati huo chama hakikuwa na ruzuku walihoji hilo? Ndiyo, nasema huo ni ujinga tu, hoja zao za kipuuzi puuzi tu, Profesa si mtu wa kushindwa kuwa na Sh milioni 30, 40 hata 50,” alisema Kambaya.

Alikwenda mbali zaidi na kuzungumzia suala la akaunti ya CUF, akipinga taarifa zinazodai kuwa ipo chini ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika hilo alisisitiza kuwa suala la fedha lipo chini ya chama na linasimamiwa na Bodi ya Wadhamini.

“Ndiyo maana nasema ujinga kwa sababu hata hiyo akaunti ya CUF haipo chini ya Katibu Mkuu, akaunti haiwezi kuwa chini ya Katibu Mkuu, kwani Katibu Mkuu ndiyo chama? Akaunti iko chini ya chama, kwani akifa huyo Seif ndiyo chama hiki hakiendi? Kwamba ameshakufa yeye na akaunti anayo yeye kwa hiyo chama hakipo?

“Ninachosema Profesa ana uwezo yeye mwenyewe wa kifedha na kakisaidia sana chama hiki. Na hii bajeti ya juzi ni Sh milioni tatu, hivi milioni tatu Lipumba hana?

“Profesa hakuanza leo kukisaidia chama, haya magari sita yaliyoingia kwenye kampeni alikopesha pesa zake dola elfu 50, mbona hawasemi? Kwa sababu ya mambo ya kiutendaji hatuwezi kusema vitu vingi, kawanunulia Radio Mwambao iko Tanga kwa kuwakopesha dola elfu 50 nyingine, mbona hawahoji? Na sijui kama wamemrudishia hizo fedha na ujue fedha hizo si za madafu, dola elfu 50 ni takribani Sh milioni 100 na ushee, mbona watu hawahoji hilo?” alisema Kambaya.

Wakati Kambaya akisema hayo, hivi karibuni yaliibuka mabishano kuhusu uamuzi wa Profesa Lipumba kutaka kufungua akaunti nyingine ya chama hicho.

Mazingira hayo pia yalimsukuma Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro, kufafanua kwamba wenye mamlaka halali ya kufungua akaunti ya chama hicho ni bodi yake ya wadhamini pamoja na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif.

“Tunatoa onyo kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kwamba tumeshafungua shauri na utaratibu wa kisheria umeshaanza kuchukua mkondo wake, tumesikitika kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, kinyume cha sheria namba tano 1992 ya vyama vya siasa na kinyume cha katiba, Msajili kwa mara ya kwanza anaziandikia benki zilizosajiliwa na BoT akizitaka kumfungulia akaunti Lipumba za kuwekea fedha,” alisema Mtatiro.

Alidai kuwa benki itakayomfungulia akaunti Lipumba itakuwa inafanya makosa makubwa.

“Kwa sababu huwezi kufungua akaunti ya taasisi au chama bila bodi yake ya wadhamini kukaa kikao na kuandaa muhtasari kwa ajili ya kupeleka benki ili kufungua akaunti. Lipumba na watu wake wameandaa nyaraka feki pamoja na barua ya Msajili kutaka kufungua akaunti. Tunajua amepeleka katika benki mbalimbali.

“Benki ya National Microfinance (NMB), ilikataa, sasa wanapeleka benki ya Exim na ilishapewa taarifa kuwa uhuni huu haukubaliki na masuala ya fedha yako chini ya katibu mkuu kwa mujibu wa Katiba ya CUF,” alikaririwa Mtatiro.

Source: Mtanzania
ZeroDegree.
Utata mamilioni ya Prof. Lipumba Utata mamilioni ya Prof. Lipumba Reviewed by Zero Degree on 10/23/2016 11:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.