Loading...

Bunge lapitisha muswada wa Sheria ya Habari.

MUSWADA wa Sheria ya Huduma za Habari umepitishwa na Bunge huku serikali ikieleza kuwa lengo la kutungwa kwa sheria hiyo ni kupunguza udhibiti wake kwenye vyombo vya habari, kwa kumpunguzia mamlaka ya kutoa adhabu Waziri anayehusika na habari pamoja na kuweka maslahi bora kwa wanahabari.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitoa maelezo hayo wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu muswada huo, ambapo kwa zaidi ya miaka 20 umekuwa ukipigwa danadana.

Michango na hoja za wabunge zilizowasilishwa ni zaidi ya 94 zikiwemo hoja 28 zilizotolewa na upande wa upinzani na hoja 30 zilizowasilishwa na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya jamii.

“Muswada huu ni tofauti na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 kama baadhi ya wabunge walivyosema tumechukua kila kitu cha sheria hiyo, ni kweli yapo mazuri tumechukua kwani kuna ubaya kuendelea nayo lakini muswada huu haumpi waziri mamlaka makubwa kama ilivyo Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976. “Serikali inataka kupunguza udhibiti wake kwa vyombo vya habari pamoja na mamlaka makubwa aliyokuwa nayo waziri kwenye sheria ya magazeti, ndio maana mamlaka hayo tumeyapeleka kwenye Baraza la Habari na huko kutaundwa Kamati ya Malalamiko, tofauti na ilivyo sasa malalamiko yanapelekwa Idara ya Habari (Maelezo) nao wanapeleka kwa waziri anayefungia gazeti,” alisema.

Alisema mamlaka aliyobakishiwa waziri kwenye muswada huo, uliopitishwa ambao Rais John Magufuli aliahidi kuusaini utakapofika tu mezani kwake, ni kuhusu makosa ya usalama wa taifa na afya ya jamii.

“Mamlaka ya zamani yalinipa mamlaka kufuta gazeti mfano nililiadhibu gazeti la Mawio na nikaadhibu wasiohusika kama wahasibu na wanasheria, lakini sheria hii mpya inahusika na mwanahabari na taaluma yake tu ambao wanakuwepo wachache wakorofi ili tusiwaathiri wengine waliopo kwenye vyombo vya habari,” alifafanua.

Alisema muswada huo uliopitishwa jana, umezingatia mabadiliko ya teknolojia na ndiyo sababu sasa mmiliki wa mtambo wa kuchapia magazeti, hataadhibiwa pindi gazeti linapokuwa na habari yenye makosa, isipokuwa pale itakapothibitika amehusika kwa makusudi.

Alisema muswada huo umemlinda mwanahabari kwa kumlazimisha mmiliki wa chombo cha habari, kutoa mikataba ya ajira, kumkatia bima ya mazingira magumu na ya afya na kuwepo chombo cha mafunzo cha kuwaendeleza wanahabari, tofauti na zamani ambapo alisema ‘wakijiendeleza wenyewe kama kuku wa kienyeji’.

Akitetea zaidi muswada huo ulivyomsaidia mwanahabari, waziri huyo alisema litakuwepo Baraza Huru la Habari, litakaloundwa na wanahabari wenyewe na hakutakuwa na mkono wa waziri.

“Baraza halitapewa fedha na serikali, hivyo litakuwa huru, si sasa MCT (Baraza la Habari Tanzania) ni kama NGO na linapata mabilioni ya fedha na huko watu wanatetea ulaji kwa mgongo wa waandishi, wanahabari watajitungia kanuni wenyewe , code of ethics zao na hata Bodi wajumbe wake saba, wanne wanahabari watatokana na wenyewe,”alifafanua.

Kuhusu ushiriki wa wadau wa habari kwenye muswada huo, Nape alisema si kweli kwamba hawajashirikishwa, kama inavyodaiwa na baadhi ya wabunge wa upinzani, bali walishiriki kwenye hatua ya kabla muswada kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri, wakati ukiandaliwa na baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni na kupelekwa kwenye kamati.

Naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura alisema kwenye muswada huo, vyombo vya habari pekee ndivyo vitatakiwa kukata leseni na si wanahabari kama ilivyodhaniwa na wengi, bali wao watapata vitambulisho kupitia kwenye Baraza la Ithibati.

Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanahabari, alisema sheria hiyo mpya itarudisha weledi wa wanahabari na waweze kulipwa vizuri, tofauti na sasa baadhi ya vyombo vya habari vinawalipa mishahara midogo wanahabari.

Waziri Nape aomba ushirikiano.


Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kupitishwa muswada huo, Nape amewaomba wadau wa habari kuisaidia serikali kwenye utungaji wa kanuni za sheria hiyo pamoja na kuwataka wanahabari walioonesha kujigawa kutokana na muswada huo, kuungana tena kuijenga tasnia ya habari.

“Serikali ipo tayari kuwashirikisha wadau wa habari kwenye utungaji wa kanuni na tunaamini haitachukua muda mrefu kukamilishwa kwa kanuni hizo na pia ifahamike utekelezaji wa sheria hiyo utahitaji ushirikiano,” alisema.

Nape pamoja na kuwashukuru wadau wa habari, walioshiriki kusaidia kufanikisha safari ya miaka 23 ya utungwaji wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 na kufanya kazi hiyo kuwa nyepesi kwa upande wa serikali.

“Mchakato ulionesha dalili ya kugawa tasnia, tutafute namna ya kuirudisha tasnia pamoja. Tuzike tofauti zetu, tukae pamoja tujenge tasnia... nawaomba tusahau tofauti zetu,” alisema.

ZeroDegree.
Bunge lapitisha muswada wa Sheria ya Habari. Bunge lapitisha muswada wa Sheria ya Habari. Reviewed by Zero Degree on 11/06/2016 07:00:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.