Loading...

Fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kuwasirishwa vyuoni leo.

Wakati ikiendelea na mchakato wa uhakiki wa waombaji wa mikopo, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB) imeagizwa kuhakikisha kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo zinapelekwa vyuoni leo.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametoa agizo hilo baada ya wabunge mbalimbali kuomba miongozo kwa Spika kuhusu kuwapo kwa wanafunzi wengi waliokosa mikopo kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Mwongozo kwa Spika ulitiliwa mkazo na Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwan Kikwete aliyeeleza kuwapo taarifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa wanafunzi wanataka kugoma kwa kukosa fedha za mikopo.

Kutokana na miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga ameitaka Serikali kutoa maelezo.

Akitoa kauli ya Serikali, Profesa Ndalichako amesema fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi zilikwenda vyuoni wiki moja iliyopita.

“Tatizo lililotokea kwa UDSM sijui kama walidanganyana au la lakini hawakujaza fomu. Serikali haitatoa mkopo kwa mwanafunzi ambaye hajajaza fomu. Na waliosaini leo wataingiziwa fedha zao kwenye akaunti na vyuo,”amesema.

Kuhusu wanaoendelea na masomo, Profesa Ndalichako amesema wanafunzi wote wanufaika na wanaoendelea na masomo wataendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa mwaka uliopita.

Hata hivyo, amesema taratibu za kuwabaini wanafunzi wenye sifa zinaendelea na wasio na sifa wataendelea kuondolewa kupata mikopo.

Pia, amekiri kuwa ucheleweshaji wa matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo umeathiri kasi ya kutuma fedha vyuoni.

Ndalichako amesema hadi kufikia Novemba 3 mwaka huu, Sh71.042 bilioni zimekwishatumwa vyuoni kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.

ZeroDegree.
Fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kuwasirishwa vyuoni leo. Fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kuwasirishwa vyuoni leo. Reviewed by Zero Degree on 11/05/2016 10:07:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.