Loading...

Simba yafanya kufuru kwa Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

SIMBA imefanya kufuru baada ya kumpa mkataba mnono wenye thamini ya Sh milioni 60, beki wake wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ili kuendelea kuitumikia klabu hiyo.

Tshabalala, aliyesajiliwa na klabu hiyo katika misimu mitatu ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akitokea Kagera Sugar, anatarajia kusaini mkataba huo mpya kesho.

Katika mkataba wake wa awali uliodumu kwa miaka mitatu, ulikuwa wa thamani ya Sh milioni 12,000, sawa na ongezeko la Sh milioni 48,000 katika mkataba mpya wa miaka miwili utakaomalizika 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa mchezaji huyo, Heri Mzozo, alisema masuala yote ya msingi kati ya pande hizo mbili yamemaliza kwa asilimia 80, hivyo kusubiri kutia saini mkataba mpya.

Mzozo alisema kabla ya kufikia dau hilo, Simba walikuwa wametoa ofa ya Sh milioni 40, lakini kwa upande wao, walisimamia dau la Sh milioni 60, ikiambatana na marupurupu kadhaa ambayo alikataa kuyaweka wazi kwa sasa.

Alisema akiwa ni meneja wa mchezaji huyo, ameamua kumbakisha Simba kutokana na umri wake kuwa bado mdogo, ili aendelee kukuza kipaji chake ndani ya klabu hiyo, ambayo imeonekana dhahiri kama nyota yake iko huko.

“Kwakweli ndani ya mkataba huu hakukuwa na matatizo, japo inawezekana kama binadamu wakatofautiana kidogo, isipokuwa msingi unabaki palepale kuwa alikuwa na maisha mazuri ndani ya timu hiyo na mimi sijaona sababu ya kumhangaisha mchezaji, tamaa pia si nzuri, ni vema ukaheshimu utu,” alisema.

Akizungumzia sababu za kuingia mapema mkataba mpya ilhali ule wa zamani unamalizika Juni 2017, Mzozo aliweka wazi ni kutaka kumaliza usumbufu ambao wamekuwa wakiupata kutoka kwa timu nyingine zikitaka kumweka sawa ili muda ukifika atie saini katika moja ya klabu hizo.

“Timu nyingi zilishaanza usumbufu, nami nafahamu wazi sheria, hatukuruhusiwa kufanya mazungumzo na timu yoyote kwa vile muda huo ilikuwa bado, hivyo ili kukata mzizi wa fitina, nimeona bora tumalizane na mwajiri wake wa sasa, kwani hata kijana bado anafurahia maisha ndani ya klabu hiyo.

“Ipo mifano ya wengi waliopotea stepu, hivyo sikutaka mchezaji wangu naye aje apotee kutokana na kuchanganywa katika vishawishi vinavyoweza kumfanya asicheze mpira. Tshabalala bado mdogo, ana uwezo, pia umri unamruhusu kucheza muda mrefu, hivyo ninataka atimize ndoto zake,” alisema.

Kusaini mkataba kwa mchezaji huyo kutamaliza hofu iliyoanza kutawala miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo, kama huenda angetimka na kuiacha kwenye mataa timu yake ambayo hivi sasa inapambana kutwaa ubingwa ilioukosa kwa misimu mitatu sasa.

ZeroDegree.
Simba yafanya kufuru kwa Mohamed Hussein 'Tshabalala'. Simba yafanya kufuru kwa Mohamed Hussein 'Tshabalala'. Reviewed by Zero Degree on 11/18/2016 12:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.