Loading...

Wachezaji nchini Tanzania ni legelege, George Lwandamina.

KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, George Lwandamina amekanusha taarifa za kuleta wachezaji kutoka Zesco lakini pia amekiri wachezaji wa Tanzania ni legelege ukilinganisha na wale wa Zambia.

Lwandamina aliyasema hayo jana wakati akitambulishwa rasmi kwa waandishi wa habari pamoja na Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Hans Pluijm.

Lwandamina alisema hana mpango wa kubadilisha chochote kwenye benchi la ufundi pamoja na wachezaji huku akikanusha kuwaleta nchini wachezaji Jesse Were na Misheck Chaila, lakini akasema amekabidhiwa jukumu zito ila analichukulia kama changamoto kuhakikisha Yanga inafanya vema.

“Nitapambana kuhakikisha Yanga inafanya vizuri, najua ni changamoto mpya kwangu, lakini nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunafanya vizuri kuanzia kwenye ligi ya nyumbani hadi klabu Bingwa Afrika,” alisema Lwandamina.

"Nasikia tetesi kuhusu wachezaji wapya kutoka Zesco kusajiliwa Yanga, naomba ifahamike kuwa kama kocha mkuu sijui chochote labda mchakato huo unafanyika bila mimi kushirikishwa, kwani kikosi kilichopo ndicho nitaendelea nacho," alisema Lwandamina.

Pia Lwandamina alisema hakuna wachezaji aliowaleta japo amekiri wachezaji wa Tanzania hawako fiziki kama wa Zambia kwani alishawaona wakati wakicheza na Ruvu Shooting kwenye mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Akimzungumzia mtangulizi wake, Lwandamina amemsifu Pluijm kwa kusema amefanya kazi nzuri na kuahidi kufuata nyayo zake kwa kushirikiana naye bega kwa bega kuhakikisha Yanga inapata mafanikio zaidi.

Mkurugenzi mpya wa ufundi, Pluijm alisema yeye hana shida na kubadilishiwa majukumu kikubwa ataendelea kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba wake. Pluijm alianza kuifundisha Yanga 2014 na ameiongoza katika mechi 128 kwenye awamu mbili, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23.

Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.

Pluijm amehamishwa katika nafasi yake ya ukocha akiwa amebeba mataji yote matatu msimu uliopita, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).

Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 walipofikia hatua hiyo katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Na kwa mafanikio hayo, Pluijm alishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita.

Wakati huo huo, timu ya Yanga itaanza rasmi mazoezi yake ikiwa chini ya kocha huyo mpya kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

ZeroDegree.
Wachezaji nchini Tanzania ni legelege, George Lwandamina. Wachezaji nchini Tanzania ni legelege, George Lwandamina. Reviewed by Zero Degree on 11/26/2016 10:29:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.