Loading...

Mtoto wa dara la 5 ajinyonga kwa kutumia shuka baada kupata matokeo mabaya katika mtihani.

MWANAFUNZI wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kizota Manispaa ya Dodoma, Yassin Abdallah (13), amejinyonga kwa kutumia shuka bafuni baada ya kupata matokeo mabaya ya mitihani yake ya mwisho wa mwaka.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Ernest Kimola, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo lililotokea juzi saa 6:00 mchana katika mtaa wa Kizota Relini, Manispaa ya Dodoma.

Kamanda Kimola alisema baba mzazi wa marehemu, Hassan Juma (53), aligundua mwanawe amejinyonga kwa kutumia shuka.

“Marehemu alikuwa akisoma darasa la tano Shule ya Msingi Kizota. Sababu za kukatisha uhai wake ni kutokana na matokeo ya mwisho ya darasa lake la tano hayakuwa mazuri,” alifafanua Kamanda Kimola.

Diwani wa Kata ya Kizota, Yaredi Jamal, alisema siku ya tukio alikuwa kwenye kikao na alipokea simu kutoka kwa Mwenyekiti wa mtaa akimtaarifu kujinyonga kwa mwanafunzi huyo.

“Nililazimika kukatisha kikao na kwenda nyumbani ambako tukio hili limetokea na nikajaribu kuuliza tatizo nini?, Nilijibiwa ni matokeo ya mitihani ndiyo yamesababisha ajinyonge,” alisema Diwani Jamal.

Alisema kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo,alikuwa ana miezi miwili tangu ahamie katika shule hiyo akitokea mkoani Kigoma.

Alisema inadaiwa mtoto huyo katika matokeo yake ya mwisho alishika nafasi ya 128 kati wanafunzi 132, hali ambayo inadaiwa ilimstua na kuamua kujinyonga.

“Hapo shuleni kaanza masomo mwezi wa 11 kwa mujibu wa walimu, ambapo kila akifundishwa na walimu alijiona haelewi kutokana na kuwakuta wenzake wakiwa wamemtangulia katika masomo wanayofundishwa," alisema Diwani Jamal.

Kufuatia hali hiyo, Diwani Jamal alitoa rai kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao na kuepuka kutoa vitisho ambavyo vitawasababisha wachukue maamuzi magumu.

“Nimeongea na wazazi wake wanasema hawajawahi kuzungumza lolote na walitambua mtoto wao anatoka kijijini anakuja kukutana na watoto wa mjini ambao uelewa wao ni tofauti. Walitarajia hadi mwakani mtoto wao angekuwa ameanza kuelewa masomo aende sawa na wenzake,” alisema Diwani Jamal.

Alisema tukio hilo limemsikitisha na halijawahi kutokea mtoto mdogo kufikia uamuzi wa aina hiyo, hivyo ni vyema wazazi wakawa karibu na watoto wao kitaaluma.

ZeroDegree.
Mtoto wa dara la 5 ajinyonga kwa kutumia shuka baada kupata matokeo mabaya katika mtihani. Mtoto wa dara la 5 ajinyonga kwa kutumia shuka baada kupata matokeo mabaya katika mtihani. Reviewed by Zero Degree on 12/05/2016 06:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.