Loading...

ATCL yaanza safari za kwenda Dodoma, ..ijue nauli ya kutoka Dar hadi Dodoma hapa

NDEGE mpya aina ya Bombardier Q400 imeanza safari za Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kuboresha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), itoe huduma bora na kwa bei nafuu.

Kutokana na kuanza kwa safari za ndege hiyo jana, sasa kutakuwa na ratiba ya safari mara mbili kwa wiki kutoka Dar es Salaam kupitia Dodoma hadi Kigoma.

Majaliwa alisema hilo ni tukio la kihistoria na mwendelezo wa uboreshaji wa makao makuu ya nchi. Alisema njia ya ndege itaendelea kuboreshwa mara wananchi walio karibu na uwanja wa ndege watapolipwa fidia ili kuwezesha ndege kubwa zaidi zitue.

“Tunafungua fursa zaidi na kuipa hadhi Dodoma kama makao makuu ya nchi,” alieleza Majaliwa.

Alisema moja ya ahadi aliyotoa Rais John Magufuli wakati wa kampeni ni kuboresha ATCL ili kutoa huduma bora na kwa bei nafuu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ni Sh 180,000 kwa safari moja ikiwa ni bei nafuu kulinganisha na mashirika mengine. Pia alisema Juni mwaka huu, serikali italeta ndege nyingine kubwa ambayo itaongeza ubora wa usafirishaji wa ndege nchini.

“Watumishi wa serikali, wafanyabiashara watumie ndege zetu serikali inahakikisha huduma zitakuwa bora na nzuri,” alisema na kuwataka ATCL kujipanga kwa ajili ya kuboresha huduma ili matumaini ya wananchi wa Dodoma yawe ya kweli.

Alisema Dodoma bado kuna nafasi ya kujengwa uwanja wa kimataifa eneo la Msalato. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema Serikali ya Awamu ya Tano inadhihirisha na kutekeleza yote iliyoahidi watanzania na kila jambo waliloahidiwa litatekelezwa.

“Ndege zitanunuliwa na kwenda maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania,” alieleza. Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela alisema serikali imefanya jambo kubwa kuboresha usafiri wa kisasa mkoani Dodoma.

Alisema serikali ielewe watu wa Dodoma wanafurahia sana kuanza kwa safari za ndege za ATCL. Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema jambo hilo limeandika historia mpya katika mkoa wa Dodoma kwani kutakuwa na usafiri wa kisasa na wa haraka.

“Juhudi hizi ni kuimarisha Dodoma kuwa makao makuu ya nchi na wana Dodoma watumie fursa hiyo vizuri,” alieleza Ndugai.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustine Kamuzora alisema matengenezo makubwa yalifanyika katika Uwanja wa Ndege Dodoma kwa ajili ya kuwezesha ndege kubwa kutua.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema tangu Rais afanye maamuzi ya serikali kuhamia Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa kiongozi wa kwanza kuhamia Dodoma na uamuzi wa kuleta ndege Dodoma ni kitendo cha ujasiri.

Alisema jambo hilo linaiweka nchi katika mazingira yatakayosaidia kukuza biashara ya utalii kwa ujumla. Mhandisi Emmanuel Korosso ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Ndege Tanzania alisema ahadi ya Rais kufufua ATCL imetekelezeka ambapo Juni mwaka huu watapata ndege nyingine ambayo itasaidia kupanua wigo. Safari za Dodoma zitakuwa kila siku za Jumatatu na Ijumaa.

ZeroDegree.
ATCL yaanza safari za kwenda Dodoma, ..ijue nauli ya kutoka Dar hadi Dodoma hapa ATCL yaanza safari za kwenda Dodoma, ..ijue nauli ya kutoka Dar hadi Dodoma hapa Reviewed by Zero Degree on 1/17/2017 10:12:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.