Loading...

Kampuni iliyopewa kazi ya kushona sare za polisi ni hewa

SAKATA la kukwama kwa zabuni ya ununuzi wa sare za Jeshi la Polisi licha ya malipo kukamilika limeibua mapya baada ya kubainika kuwa kampuni iliyopewa kazi hiyo ni hewa.

Mbali ya kwamba ni kampuni ya mfukoni, pia imebainika kuwa taarifa za awali zilionyesha inajihusisha na uuzaji wa vifaa vya ujenzi. 

Ufisadi wa kampuni hiyo inayodaiwa kuingia mitini licha ya kulipwa kati ya Sh. bilioni 40 na Sh. bilioni 60 kwa ajili ya kununua sare za Polisi ulifichuliwa na Rais John Magufuli Julai 18, mwaka jana wakati akiwaapisha makamishna wa Jeshi la Polisi waliopandishwa vyeo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, amethibitisha kwamba kampuni hiyo ni hewa kwa sababu wameshindwa kubaini zilipo ofisi zake.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum, Jenerali Rwegasira alisema awali waliambiwa Daissy General Traders ina ofisi katika makutano ya mitaa ya Uhuru na Swahili, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Kutokana na maelezo ya hayo katika anuani ya kampuni hiyo, Rwegasira alisema, waliafuatilia ili kujiridhisha kama ziko sehemu hiyo, alisema.

Lakini walipofika, alisema zaidi Jenerali Rwegasira, hawakukuta ofisi hizo, jambo ambalo limewafanya wakabidhi kazi hiyo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili ichunguze zaidi.

Julai 18, mwaka jana, alipokuwa akiwaapisha Manaibu Kamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi (SACP) wa jeshi hilo, Rais Magufuli alisema amepata taarifa za rushwa ndani ya Jeshi la Polisi inayokadiriwa kuwa kati ya Sh. bilioni 40 na Sh. bilioni 60 ambazo zilipaswa kununulia sare kwa ajili ya askari polisi tangu mwaka 2015, lakini hazijanunuliwa.

Rwegasira alisema taarifa walizozipata awali zilikuwa zikionyesha kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikijihusisha na masuala ya uuzaji wa vifaa vya ujenzi.

KWA TAKUKURU

Katibu mkuu huyo alisema kuna uwezekano kwamba kuna watu walipeana zabuni hiyo na kampuni ambayo ni ya mfukoni isiyokuwa hata na ofisi, ndiyo maana wameshindwa kuipata ilipo.

Inadaiwa kuwa kampuni hiyo iliingia mikataba na Polisi kati ya mwaka 2013-2016, lakini katika kipindi chote hicho imeshindwa kusambaza hata sare moja.

Kutokana na kuwapo mazingira ya utata, Rwegasira alisema kuanzia Agosti 18, mwaka jana, aliamua kukabidhi kazi hiyo kwa Takukuru ili kuchunguza mikataba iliyotolewa kwa kampuni hiyo kati ya 2013 na 2016.

“Takukuru na wenyewe wana muda wao katika kuchunguza jambo hilo, hivyo kama unahitaji taarifa kwa zaidi nenda Takukuru watakusaidia,” alisema Jenerali Rwegasira.

Msemaji wa Takukuru, Mussa Msalaba, alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema wanaendelea kuchunguza na kwamba upelelezi ukikamilika taarifa itatolewa.

Rais Magufuli alilitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vilinafanya kukosa heshima katika jamii, siku hiyo.
Alisema ana taarifa za jeshi hilo kuingia katika makubaliano ya kifisadi ya mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kununua sare za jeshi hilo.

Rais Magufuli alisema ni jambo la kusikitisha kwamba mabilioni hayo yalitolewa kwa siku moja lakini hadi Julai 18, mwaka jana hiyo, hakukuwa hata na sare moja ya iliyonuuliwa.

Kipindi hicho kimeongezeka kwa miezi sita zaidi sasa.

Katika hafla hiyo, Rais alishangazwa na jeshi hilo kutoa kiasi cha fedha wakati Polisi ikikosa Sh. bilioni nne tu za kukomboa magari zaidi ya 70 yaliyokuwa yakishikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) bandarini kutokana na kutolipiwa kodi.

Aidha, Rais Magufuli aliagiza uchunguzi ufanyike na wahusika wafikishwe mbele ya haki ili angalau hata nusu ya fedha hizo ziweze kurudishwa zikalipie ushuru wa magari ya polisi yaweze kutoka bandarini, lakini sasa imegundulika kampuni hiyo ni hewa na pengine fedha hizo haziwezi kurudi si tu angalau nusu bali zote.

KAMPUNI YA LUGUMI

Tangu Magufuli aapishwe kuwa Rais wa Tano Novemba 5, mwaka 2015, mikataba kadhaa tata imegundulika katika Jeshi la Polisi.

Mbali na mkataba huo wa kati ya Sh. bilioni 40 na Sh. bilioni 60 kwa ajili ya kununua sare, Polisi imechafuliwa pia na mkataba kati yake na Kampuni ya Lugumi Enterprises kuhusu mradi wa utambuzi wa alama za vidole (AFIS) wenye thamani ya Sh. bilioni 37 ambao unakabiliwa na hofu ya kujaa ufisadi pia.

Katika mkataba huo ambao kwa sasa unasubiri maamuzi ya Bunge baada ya uchunguzi wa kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kampuni ya Lugumi ilitakiwa kufunga mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo vya polisi 108.

Lakini habari za awali zilieleza kuwa ni vituo 14 tu ndivyo vilivyokuwa na mashine hizo mpaka Aprili mwaka jana, wakati kampuni hiyo ililipwa Sh. bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote tangu 2013.

Ni mazingira hayo yaliyoifanya PAC kuhitaji kupatiwa mkataba huo ili kuupitia.

Ilidaiwa pia kuwa kati ya vituo 14 hivyo vilivyokuwa vimefungwa mashine hizo za kieleketoriniki, ni vinane tu ndivyo vilikuwa vikifanya kazi, hali iliyofanya kamati ndogo ya PAC kuzunguka nchi nzima kufuatilia utekelezaji wa mkataba huo.

Mkataba wa Lugumi unaelezwa kuwa kaa la moto, hata hivyo, baada ya mtoto wa mmoja wa marais wastaafu na IGP mmoja mstaafu kutajwa kuwa washirika wa kibiashara wa mmoja wa wamiliki wawili wa kampuni hiyo, Said Lugumi.

Awali akifungua kikao kazi cha Jeshi la Polisi katika Ukumbi wa Mikutano wa Dodoma Aprili 29, mwaka jana, Rais alilitaka kuacha kuingia mikataba yenye mashaka, akigusia pia makubaliano kati yake na mwekezaji katika eneo la Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli alisema kama angekuwa yeye, angeendeleza eneo hilo kwa kukopa fedha za ujenzi wa jengo la kitega uchumi benki kwa kutumia hati ya eneo hilo la Kituo Kikuu cha mkoa wa kipolisi wa Kinondoni.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Kampuni iliyopewa kazi ya kushona sare za polisi ni hewa Kampuni iliyopewa kazi ya kushona sare za polisi ni hewa Reviewed by Zero Degree on 1/14/2017 03:18:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.