Loading...

Mhasibu TRA makao makuu ahukumiwa kifungo cha miaka 5 jela

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, imemhukumu aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Justice Katiti, na wenzake wanne kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh. milioni 100 kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya rushwa na utakatishaji fedha haramu.

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Renatus Rutatinisibwa, alitoa hukumu hiyo Januari 17, mwaka huu baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilisema jana.

Hakimu Rutatinisibwa aliwatia hatiani washtakiwa kwa jumla ya makosa 51 ya rushwa na utakatishaji wa fedha haramu yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Takukuru Julai 21, 2010.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Takukuru iliyotolewa na Ofisa Uhusiano wake Mussa Misalaba, washtakiwa walipelekwa gerezani kuanza kutumikia kifungo hicho, baada ya kushindwa kulipwa faini ya Sh. milioni 100 kila mmoja.

Washtakiwa wengine walioanza kutumikia kifungo pamoja na Katiti ni Marcus Masila ambaye alikuwa Mhasibu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Kanuti Ndomba, mfanyabiashara wa kampuni ya UEE Tanzania Ltd.

Wengine waliohukumiwa kifungo hicho cha miaka mitano au kulipa faini ya Sh. milioni 100 ni Gideon Otullo ambaye ni mfanyabiashara wa kampuni ya East Africa Procurement Services na Robert Mbetwa, mfanyabiashara wa kampuni ya Romos Technology Co. Ltd.

Taarifa ya Misalaba ilisema kesi hiyo iliendeshwa na waendesha mashtaka toka ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na Takukuru ambao ni Awamu Mbagwa (DPP), Shedrack Kimaro (DPP), Estazia Wilson (DPP) na Marx Ally (Takukuru).

Kwa kuwa kosa la kutakatisha fedha haramu halina dhamana kisheria, Katiti na wenzake wanne walikuwa mahabusu kwa zaidi ya miaka sita iliyopita.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Mhasibu TRA makao makuu ahukumiwa kifungo cha miaka 5 jela Mhasibu TRA makao makuu ahukumiwa kifungo cha miaka 5 jela Reviewed by Zero Degree on 1/21/2017 10:33:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.